Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 20:10

Wakimbizi watano wauwawa nchini Rwanda


Wakimbizi ambao wanaishi katika kambi ya wakimbizi ya Kiziba huko Wilaya ya Karongi, Rwanda, Februari 21, 2018.
Wakimbizi ambao wanaishi katika kambi ya wakimbizi ya Kiziba huko Wilaya ya Karongi, Rwanda, Februari 21, 2018.

Raia wa Kongo watano wameuwawa Ijumaa wakati jeshi la polisi la Rwanda na jeshi la wananchi walipotumia risasi za moto kuwatawanya wakimbizi ambao walikuwa wameweka kambi nje ya ofisi za Umoja wa Mataifa zinazoshughulikia masuala ya wakimbizi huko magharibi ya Rwanda.

Tamko lilotolewa na Polisi wa Rwanda limesema “ Tulitumia nguvu za kadri ambazo zilipelekea watu 20 waliokuwa wanaleta vurugu na maafisa polisi kadhaa kujeruhiwa. Wote hao walipelekwa hospitali mara moja. Bahati mbaya watu watano kati ya wale waliokuwa wanaleta vurugu walipoteza maisha kutokana na majeraha hayo."

Polisi wamesema wamewakamata wakimbizi 15, kwa tuhuma za kuandaa maandamano kinyume cha sheria, kuwateka watu na kuchochea vurugu.

Wakimbizi wanasema idadi ya vifo inaweza kuwa iko juu kuliko ile iliotolewa na polisi.

Siku ya Alhamisi, Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi (UNHCR) limetoa wito kuwepo utulivu na kujizuilia kufuatia taarifa juu ya maadamano ambayo yaliyogeuka kuwa vurugu katika kambi ya wakimbizi ya Kiziba nchini Rwanda.

Kambi hiyo katika wilaya ya Karongi inakaliwa na wakimbizi zaidi ya 17,000 ambao wamekimbia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Waandamanaji hao inaripotiwa kuwa walikuwa wamekasirishwa na punguzo la asilimia 25 la msaada wa chakula unaotolewa kwao.

“Ulinzi wa Wakimbizi na usalama wao ni kipaumbele chetu,” Ahmed Baba Fall, Mwakilishi mkazi wa UNHCR nchini Rwanda, amesema katika taarifa yake Ijumaa.

Wakimbizi hao wanashinikiza kuondolewa nchini Rwanda na kupelekwa kuishi nchi nyingine. Iwapo hilo halitofanyika, wanasema watarudi kwa kutembea kwa miguu nchini DRC.

“Wakimbizi wanahaki ya kurudi katika nchi zao wakati wowote wanapotaka. Lakini tunawasihi wakimbizi kufanya maamuzi ya busara na waache kusikiliza taarifa za uongo na uzushi,” amesema Baba Fall.

Rwanda inawahifadhi zaidi ya wakimbizi 173,000 katika kambi sita, ikiwemo ya Kiziba ambapo baadhi ya Raia wa Congo ambao wameishi zaidi ya miaka 20.

XS
SM
MD
LG