Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 07, 2024 Local time: 11:43

Kenya iko mbioni kupunguza muda wa matumizi ya dawa za Kifua Kikuu


Utafiti wa ugonjwa wa TB ukifanyika katika maabara za mtafiti mkuu katika taasisi ya matibabu na utafiti, Kenya KEMRI. Picha na Amina Chombo
Utafiti wa ugonjwa wa TB ukifanyika katika maabara za mtafiti mkuu katika taasisi ya matibabu na utafiti, Kenya KEMRI. Picha na Amina Chombo

Dunia ikiwa inaadhimisha siku ya Kifua Kikuu Ulimwenguni, Kenya iko mbioni kupunguza muda wa matumizi ya dawa za kutibu Kifua Kikuu, TB, kutoka miezi 6 hadi 4.

Taasisi ya taifa ya utafiti wa matibabu Kenya, KEMRI, imesema matokeo ya utafiti wao wa awali ulisaidia kupunguza matumizi ya vidonge vya TB kutoka miezi 18 hadi 6 , na sasa wanapania kupunguza hadi miezi minne, hayo yameelezwa katika ripoti yao kwa vyombo vya habari.

“Kupitia utafiti katika kituo hiki, lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunapata dawa ambazo zitakuwa za muda mfupi zaidi ili kumsaidia mgonjwa kuzitumia dawa na kumaliza dozi, ili kumaliza TB,” amesema Dkt Jane Ongango, kaimu mkurugenzi kituo cha utafiti wa magonjwa ya mapafu, (CRDR) KEMRI.

Aidha kituo hicho cha utafiti cha magonjwa ya mapafu kimeimarisha juhudi za majaribio ya chanjo mbili kwa ajili ya watoto wachanga na watu wazima.

Watafiti hao wakiongozwa na mtafiti mkuu Dkt Videlis Nduba wa KEMRI, kwa sasa wanashughulikia chanjo ya watoto wachanga dhidi ya TB.

Watoto wachanga zaidi ya 1500, tayari wamepatiwa chanjo za BCG recombinant kwenye majimbo ya Nairobi na Siaya, nchini Kenya.

“Tumemaliza utafiti wa chanjo ya Recombinant kwa watoto wachanga wanaozaliwa na tayari tumewasajili na kuwapatia chanjo watoto 800 Nairobi na watoto wachanga 812, huko Siaya.

Tuliwagawanya katika makundi mawili, kundi moja ni lile ambalo limepatiwa chanjo iliyoboreshwa inayoitwa BCG Recombinant na wengine walipatiwa chanjo ya kawaida ya BCG,” amesema Dkt Videlis Nduba, mtafiti mkuu katika taasisi ya matibabu na utafiti, KEMRI.

Utafiti wa ugonjwa wa TB ukifanyika katika maabara za mtafiti mkuu katika taasisi ya matibabu na utafiti, KEMRI. Picha na Amina Chombo
Utafiti wa ugonjwa wa TB ukifanyika katika maabara za mtafiti mkuu katika taasisi ya matibabu na utafiti, KEMRI. Picha na Amina Chombo

Dkt Nduba ameongeza kuwa wameteuliwa kwa awamu ya tatu ya utafiti wa kuzalisha chanjo dhidi ya TB kwa wasichana na watu wazima kwa lengo la kuwachanja wale ambao tayari wameugua TB, ili kuzuia maambukizi ya mara ya pili ama wale ambao wanaugua magonjwa hatarishi kwa TB.

TB ni ugonjwa wa pili unao sababisha vifo miongoni mwa magonjwa yanayoambukiza baada ya COVID 19; watu milioni 1.6 waliripotiwa kufariki kutokana na TB mwaka 2021, ikiwemo watu 187, 000 wanaoishi na virusi vya HIV.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa Kenya iliripoti visa 139,000 vya maambukizi ya TB na vifo 20,000 mwaka 2020; TB ikiwa ugonjwa wa nne unaosababisha vifo katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Ili kukabiliana na changamoto ya kutambua viini vya TB kwa watoto, moja ya changamoto kote duniani, watafiti wa KEMRI kwa ushirikiano na madaktari wengine, wanafanyia kazi teknolojia mpya ili kuwasaidia kutambua maambukizi ya TB kwa watoto.

Utafiti huo utawasaidia kutambua viini kwa watoto kwa kuangalia Extracelular vesicles sawia na kuangalia kiini cha TB katika mkojo na damu.

Wakifanikiwa basi TB itagundulika haraka kwa watoto ambao wengi huchelewa kutambulika .

Wakati huo huo utafiti mwingine waendelea kutumia teknolojia ya kutumia software ambayo inaweza kubaini kama kikohozi ni cha TB na kikohozi kingine.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni ndio twaweza kumaliza TB.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amina Chombo, Kenya.

XS
SM
MD
LG