Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Oktoba 06, 2024 Local time: 00:31

Kenya Airways yapokea kibali kuingiza ndege Marekani


Ndege ya shirika la ndege Kenya Airways
Ndege ya shirika la ndege Kenya Airways

Shirika la ndege la Kenya Airways Alhamisi limepokea idhini rasmi ya kuingiza ndege za moja kwa moja nchini Marekani.

Uidhinishaji huu kutoka Usimamizi wa usalama wa usafirishaji wa Marekani (TSA) unafungua milango ya KQ kufanya uzinduzi wa safari zake kati ya Nairobi na New York Oktoba 28, 2018 na kulifanya shirika la kwanza kutoka Afrika Mashariki kuwa na safari za moja kwa moja kuja Marekani.

Barua hii ya idhini ilipokewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kenya Airways Sebastian Mikosz kutoka kwa Balozi wa Marekani nchini Kenya Robert Godec kwa niaba ya serikali ya Marekani.

Akiipokea barua hiyo Sebastian Mikosz katika hafla ambayo pia ili hudhuriwa na Waziri wa Uchukuzi James Macharia na maafisa kadhaa wa sekta ya usafiri wa anga nchini Kenya, akieleza kuwa hii ni hatua muhimu na ya mwisho kwa KQ kuingia uwanja wa JFK, New York.

‘Katika mchakato huu kuna hatua kadhaa. Si hatua tu za kibiashara bali pia hatua ambazo ni rasmi zinazo ashiria utaratibu muhimu wa kupata idhini. Tumekuwa katika mchakato huu zaidi ya miaka mitatu iliyopita na Alhamisi utaratibu muhimu umeafikiwa kwa hivyo nimeridhishwa na kufurahi sana.’alieleza Mikosz.

Ndege aina ya Boeing 787 Dreamliner zinazobeba zaidi ya abiria 335, zitachukua saa 14 kutoka Nairobi hadi New York na saa 15 kutoka New York hadi Nairobi kwa kutumia marubani wanne na wahudumu 12.

Balozi wa Markeni nchini Kenya, Robert Godec anaeleza kuwa kukabidhiwa idhini hii rasmi Kenya Airways, ni ishara ya mashauriano mapana yenye ufanisi na mahusiano bora kati ya Nairobi na Washington.

‘Barua hii inaupa uwanja wa ndege wa kimataifa Jomo Kenyatta idhini rasmi ya kuwa kituo cha mwisho mno kwa ndege za Kenya Airways kuondoka Kenya kuingia Marekani.

Na hizi safari za moja kwa moja zitakapoanza mwisho wa Oktoba zitarahihisha usafiri kati ya nchi zetu mbili,zitaunganisha watu wetu. Itakuwa rahisi kwa wafanyabiashara wetu, watalii, maafisa wa serikali zetu na vile vile wanafunzi kusafiri.’alisema Bw Godec.

Kenya ilipewa masharti ya kudumisha usalama katika uwanja wa ndege JKIA, kuwahakikishia wasafiri usalama wao na vile vile kufanya mageuzi muhimu katika sekta ya usafiri wa anga.

Februari,2017, Kenya ilipewa hadhi ya kwanza almaarufu Category one Status na serikali ya Marekani. Kati ya Julai na Agosti 2017, KQ lilipokea hati za haki za trafiki za Marekani kuingiza ndege zake uwanja wa ndege wa JFK, New York na October,2017, uwanja wa ndege wa JKIA ulifanyiwa ukaguzi na idara inayosimamia safari za anga ya Marekani FAA kabla kuwezeshwa kuwa kituo cha mwisho cha ndege zake kuondoka Kenya.

Hata hivyo, Marekani imetangaza ufadhili mpya kwa mamlaka ya viwanja vya ndege nchini Kenya (KAA) kuimarisha usalama.

“Kama njia ya kufanikisha safari za ndege za moja kwa moja na vile vile kuimarisha usalama wetu, serikali ya Marekani inatangaza kuongeza ufadhili za ziada wa $1.5 milioni kwa mamlaka ya viwanja vya ndege nchini Kenya kununua vifaa ziada vya usalama na kwa ajili ya mafunzo. Hii itahakikisha abiria wanakuwa salama.”aliongeza Godec.

Akizungumza katika hafla hii, Waziri wa Uchukuzi James Macharia ameeleza kuwa hatua hii inaipa Kenya hadhi na hivyo basi ni jukumu la Kenya kupitia washikadau wa sekta ya usafiri wa anga Kenya kudumisha ubora huu.

“Ni sharti tuulinde na kuudumisha ufanisi huu kwa ajili ya shirika la ndege la KQ na vile vile mamlaka ya viwanja vya ndege vya Kenya na kwa nchi yetu. Ni sharti tuutunze uwanja huu wa ndege wa JKIA vizuri na kuupa fahari ya kimataifa.” Alieleza Macharia.

XS
SM
MD
LG