Ajali hiyo ilitokea Jumapili jioni wakati basi hilo lilipokuwa safarini kutoka mji wa Meru kuelekea mji wa pwani wa Mombasa. Basi hilo lilitumbukia kwenye daraja karibu mita 40 kwenye bonde la mto Nithi.
Picha zilizochapishwa kwenye vyombo vya habari vya eneo hilo zilionyesha basi hilo likiwa limepasuka baada ya kubingirika kwenye mteremko mkubwa, huku ripoti zikisema mabaki na miili ilikuwa imetapakaa majini na kwenye ukingo wa mto.
Watu 20 walifariki papo hapo siku ya Jumapili, huku wanne wakifia hospitalini na miili mingine zaidi kupatikana Jumatatu, kamishna wa kaunti Norbert Komora aliwaambia wanahabari.
Alisema Uchunguzi bado unaendelea kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Idadi ya watu waliouawa kwenye barabara za Kenya imeongezeka katika miaka ya hivi karibuni.
Katika nusu ya kwanza ya 2022, watu 1,912 waliuawa, ikiwa ni asilimia tisa kutoka 1,754 katika kipindi kama hicho mwaka jana, kulingana na takwimu za Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama.