Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Februari 01, 2023 Local time: 16:05

Kofi Annan aaga dunia


Katibu Mkuu wa zamani wa UN Kofi Annan

Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN) Kofi Annan alifariki Jumamosi asubuhi katika hospitali moja mjini Berne, Uswizi, baada ya kile wakfu wake ulisema ni 'kuugua kwa muda mfupi."

Annan, ambaye alishinda tuzo ya amani ya Nobel mnamo mwaka wa 2001, amefariki akiwa na miaka 80.

Taarifa iliyotolewa na wakfu wa Kofi Annan ilieleza kwamba mwanadiplomasia huyo alikuwa amezungukwa na familia yake, wakiwemo mkewe na wanawe watatu, wakati wa kifo chake.

Katibu Mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema Jumamosi kupitia ujumbe wa Twitter kwamba Annan alikuwa ni mshauri imara katika kuelekeza mambo mema.

Alisema kuwa anaungana na ulimwengu katika kuomboleza kifo chake.

"Katika nyakati hizi zenye misukosuko na majaribio mengi, urithi aliyotuachia kama dira ya amani itabakia kuwa ni hamasisho la kweli kwa sisi sote," alisema.

"Hauwezi kuutenganisha Umoja wa mtaifa na Kofi Annan," aliongeza.

Annan, ambaye alizaliwa nchini Ghana, alikuwa Mwafrika mweusi wa kwanza kutumikia wadhifa wa katibu mkuu wa UN kwa mihula miwili (1997-2006).

Mwanadiplomasia huyo alikuwa mmoja wa wapatanishi wakuu nchini Kenya katika mchakato wa kutafuta amani kufuatia ghasia zilizozuka baada ya uchaguzi ulioibua utata wa mwaka wa 2007, na kupelekea vifo vya zaidi ya watu 1,200 na umwagikaji wa damu.

Katika rambirambi zake kwa familia ya Annan Jumamosi, aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya, Raila Odinga, alimtaja kama mtu "aliyeiokoa Kenya ilipokabiliwa na uwezekano wa kusambaratika."

Kofi Annan asalimiana na rais wa DRC Joseph Kabila. Mwanadiplomasia huyo alihusika pakubwa katika michakato ya kutafuta amani barani Afrika kati ya maeneo mengine duniani.
Kofi Annan asalimiana na rais wa DRC Joseph Kabila. Mwanadiplomasia huyo alihusika pakubwa katika michakato ya kutafuta amani barani Afrika kati ya maeneo mengine duniani.

Annan aidha aliwahi kuwa mjumbe maalum wa UN nchini Syria na kushiriki katika kuleta suluhu katika mgogoro wa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Kofi Annan ilimuelezea kama kiongozi aliyejitolea kwa kiwango kikubwa katika masuala ya kimataifa. Wakati wa uhai wake wote alipigania kuwepo ulimwengu wenye amani.

Wakati wa uongozi wake Annan kama katibu mkuu alikabiliwa na changamoto nyingi kutokana na vita zilizokuwa zikiendelea na majanga mbalimbali.

Hata hiyo, Annan alishutumiwa kwamba alitumia wadhifa wake kujifaidi na kwamba alimpa mwanawe kadarasi iliyozua utata. Baadaye Umoja wa mataifa ulibaini kwamba shutuma kwama Annan alihusika kwa kashfa hiyo "hazikuwa na msingi wowote."

Wakosoaji pia walimshutumu Annan kwa kutochukua hatua zilizohitajika, kukabiliana vilivyo na vita yvya wenyewe kwa wenyewevya mwaka wa 2004 nchini Rwanda vilivyopelekea vifo vya takribani watu laki nane.

Kofi Annan akizungumza na waandishi wa habari katika moja ya mikutano.
Kofi Annan akizungumza na waandishi wa habari katika moja ya mikutano.

Annan alikiri kwamba hakulipa suala hilo umuhimu uliohitajika. "Baadaye niligundua kwamba kuna mengi ambayo tungfanya kukabiliana na janga hilo," alisema kwenye mahojiano na kituo kimoja xcha televisheni ya Marekani mnamo mwaka wa 2006.

Hali kadhalika alishutumiwa vikali kufuatia mauaji ya maelfu ya wanaume na wavulana wa Kiislamu katika mji wa Srebrenica, Bosnia, mnamo mwaka wa 1995.

Licha ya shutuma hizo, rambirambi ziliendelea kumiminika Jumamosi kutoka kwa viongozi mbalimbali duniani kote huku wengi wakimtaja kama mwanadiplomasia wa kipekee ambaye alitetea amani na umoja maisha yake yote.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG