Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Februari 06, 2023 Local time: 23:02

Jenerali Kayihura afikishwa mahakama ya kijeshi Uganda


Jenerali Edward Kale Kayihura

Mkuu wa polisi wa zamani nchini Uganda Jenerali Kale Kayihura amefunguliwa mashtaka katika mahakama ya kijeshi jijini Kampala, akihusishwa na matumizi mabaya ya ofisi ikiwemo kushindwa kulinda silaha za kijeshi na kusaidia katika utekaji nyara.

Kayihura, mwenye umri wa miaka 62 ambaye amekuwa kizuizini katika kambi ya jeshi ya Makindye jijini Kampala, tangu mwezi juni, anashutumiwa kwa kuwaruhusu watu ambao sio maafisa wa usalama, kama wanachama wa kundi la wahudumu wa boda boda 2010, likiongozwa na Abdullah Kitata, kumiliki bunduki na risasi kinyume cha sheria, wakati wa uongozi wake wa miaka 13 kama mkuu wa polisi.

Wasimamizi wa mashtaka wakiongozwa na Meja Jenerali Mugisha, wameiambia mahakama kwamba Jenerali Kayihura alishindwa kutoa hesabu kamili ya bunduki na risasi zilizo katika kila kituo cha polisi na idara zote za usalama.

Vyombo vya habari vya Uganda vimeripoti kwamba kiasi cha bunduki 4000 zilipotea wakati wa utawala wa Jenerali Kayihura, lakini msemaji wa polisi Emilian Kayima alikanusha taarifa hizo akisema hazina ukweli wowote.

Pia, Jenerali huyo amefunguliwa mashtaka ya kusaidia katika utekaji nyara kinyume na ibara ya 19 ya sheria za nchi, kwa kuwateka nyara wakimbizi wa Rwanda waliokuwa wakiishi nchini Uganda na kuwarejesha Rwanda bila kufuata sheria za nchi.

Kati ya waliotekwa nyara na kurudishwa Rwanda kati ya mwaka 2012 na 2016 ni pamoja na aliyekuwa mlinzi wa Rais wa Rwanda Paul Kagame, Luteni Joel Mutabazi, Jackson Karemera na Innocent Kariisa.

Mutabazi, aliyekuwa akiishi nchini Uganda kama mkimbizi, alirejeshwa nchini Rwanda mnamo mwaka 2013, na kufunguliwa mashtaka ya kuhatarisha usalama wa nchi.

Kayihura amekana mashtaka yote na kurejeshwa kizimbani hadi tarehe 4 mwezi septemba atakaporejeshwa tena mahakamani huku kikao cha mahakama kikisikiliza iwapo anaweza kuachiliwa kwa dhamana, kilichopangwa kufanyika tarehe 28 mwezi Agosti.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington, DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG