Wakazi wanasema wameshuhudia makombora yakidondoka karibu na kambi ya wakimbizi, makazi ya watu pamoja na misikiti. Jeshi la Israel kwa upande wake limesema kwamba lililenga ngome za magaidi ndani ya Rafah, na kwamba wakati wa operesheni hiyo wamefanikiwa kuokoa mateka wawili wa Israel wenye asili ya Argentina, waliokuwa wanashikiliwa na wanamgambo wa Hamas.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amepongeza operesheni hiyo, akisema kwamba taifa lake halitapoteza nafasi hata moja ya kurejesha mateka wanaoshikiliwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza. “ Shinikizo la kijeshi hadi ushindi, ndilo pekee litakalopelekea kuachiliwa kwa mateka wote,” amesema Netanyahu.
Zaidi ya miezi 4 ya mapigano pamoja na amri za kuondoka kwa wakazi kutoka Gaza zimewasababisha wapalestina wa kanda hiyo yote kuhamia upande wa kusini, wengi wao wakiishi kwenye makambi ya Umoja wa Mataifa, yenye misongamano mikubwa karibu na mji wa Rafah.
Forum