Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 27, 2022 Local time: 19:10

Trump ataka mabadiliko kuijenga Marekani


Wajumbe wa Congress

Akitoa hotuba yake ya kwanza mbele ya wajumbe wa Congress kwenye mkutano wa pamoja, Rais Donald Trump ameonyesha kuwepo matumaini Jumanne usiku kuliko alivyosikika katika hotuba yake ya kuapishwa wiki sita zilizopita.

“Wakati wa fikra duni umekwisha,” alitangaza. “Wakati wa vita ndogo ndogo umepita.”

Lakini amegusia juu ya vita—hasa mapambano dhidi ya kile rais alichokiita “ugaidi wa Kiislamu.”

Kauli ya Ugaidi

Hiyo ni kauli, kwa mujibu wa baadhi ya vyombo vya habari, ambayo Mshauri wa Usalama wa Taifa Luteni Jenerali H R McMaster na baadhi ya wafanyakzi wake walimshauri Trump kuacha kuitumia.

McMaster inasemekana aliwaambia wafanyakazi wa idara yake wiki iliyopita angependelea yatumike maneno “vikundi vya kigaidi” ambayo inaelezea ni wale tu wanaosaidia misimamo mikali katika Uislam- katika serikali na jamii, kuliko kutumia kauli za jumla kwamba Waislamu wote ni magaidi.

Na kwa kuhusu kikundi cha Islamic State, Trump amesema Marekani “itafanya kazi na washirika wake, wakiwemo marafiki zetu na washirika katika ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kumtokomeza adui huyu muovu kutoka duniani.

Mkutano wa pamoja wa wajumbe wa Congress
Mkutano wa pamoja wa wajumbe wa Congress

Matumizi ya Miundombinu

Rais ametangaza kutumia dola trilioni 1 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya Marekani na kulitaka Bunge kupitisha sehemu muhimu ya bajeti ya kuimarisha ulinzi.

Pia ameahidi kupunguza kodi katika biashara na kwa watu wa kipato cha kati lakini hakutoa maelezo kuhusu punguzo kubwa la bajeti katika maeneo mengine.


Punguzo hilo bila shaka katika baadhi ya maeneo ya matumizi ni kubwa na lenye utata.

Punguzo la Bajeti

Wakati kuna taarifa kwamba Wizara ya Mambo ya Nje itakuwa na punguzo la asilimia 38 katika bajeti yake, Kiongozi wa Baraza la Seneti waliowengi, Mitch McConnel, amewaambia waandishi wa habari kabla ya hotuba hiyo kuwa hatokubali punguzo hilo na wala halitopitishwa na bunge.

Mrepublikan huyo pia amesema chama chake bado hakijafikia makubaliano katika mpango wa kubadilisha Sheria ya Afya (Affordable Care Act); bima ya afya ya serikali kuu inayojulikana kama Obamacare.

Wakati analihutubia taifa Trump aliweka wazi kwamba “Obamacare inafeli—na lazima tufanye maamuzi kuwasaidia Wamarekani. …Hivyo basi nawataka Wademokrat na Warepublikan wote katika Bunge kushirikiana na sisi kuwaokoa Wamarekani kutokana na janga la hii Obamacare ambayo imefeli.

Kauli ya Wademokrati

Katika kujibu tuhuma za rais, Steve Beshear wa Chama cha Demokratik ambaye ni governor wa zamani wa Kentucky, akizungumza kutoka katika jimbo lake wakati wa chakula cha usiku, alimshutumu rais kwa kutokuwa makini.

“Wakati rais anavishambulia vyombo vyetu vya usalama vilivyo na ukweli na uaminifu, mifumo ya mahakama, jeshi, vyombo vya habari huru na baadhi wamarekani --- kwa sababu tu hajafurahishwa na kile wanachosema---anaiangamiza demokrasia yetu,” amesema Beshear.

Baadhi ya watu wanaompinga wanaiona hotuba ya rais inakosa maelezo maalum katika upande wa sera.

Sera ya Nje

“Uongozi wa Rais Trump unaonyesha kutokuwepo kabisa sera ya mambo ya nje imara. Hotuba yake usiku wa Jumanne haikufanya chochote kulitatua tatizo hilo kubwa,” amesema Michael Breen, rais wa mradi wa Truman National Security.

Rais ameelekeza lawama kwa uongozi uliopita akisema kuwa uongozi wake “umerithi mlolongo wa maafa katika sera ya mambo ya nje iliyokuwa ovyo.

Trump ameeleza ataendelea kushirikiana na NATO na tena amewataka washirika kulipa michango yao.”

Amesema kufuatia “mazungumzo ya kina na ya ukweli,” wanachama wa NATO wameanza kutoa michango yao “ Naweza kuwaambia kwamba fedha inamiminika,” Trump amesema, japokuwa hakufafanua.

Waandamanaji

Kabla kidogo ya rais kuanza kuhutubia, kulikuwa na baadhi ya waandamanaji waliokusanyika wakati mvua inanyesha huko sehemu ya Lafayette Park, upande wa pili wa White House.

Pia kulikuwa na kumpinga rais ndani ya Bunge kwa baadhi ya wanawake kuvaa nguo nyeupe, zilizokuwa zinaashiria madai ya haki zao. Wanawake walivaa nguo nyeupe katika karne ya 19 na mwanzo wa karne ya 20 kama ishara ya kushinikiza haki zao za kupiga jira.

Suala la Uhamiaji, ambalo lilikuwa likijirudia wakati wa kampeni yake ya urais, lilikuwepo katika hotuba yake lakini kwa namna tofauti: Rais akipendekeza kwamba wahamiaji wachukuliwe kwa sifa zao kama inavyo fanyika nchi nyingine.

Ahadi ya Kujenga Ukuta

Pia alirejea ahadi yake ya kujenga “ ukuta mkubwa mkubwa utaoenea upande wa kusini wa mpaka wetu,” akiahidi kwamba ujenzi utaanza karibuni. Lakini hakurudia kiapo chake kilichojirudia kwamba Mexico watalipa gharama ya ujenzi.

Kila mwaka wakati rais anapofika kwenye Bunge, kuhutubia mkutano wa pamoja- unaojulikana kama Hali ya Kitaifa wanataja ahadi nyingi—isipokuwa tu inapokuwa ni hotuba ya kwanza ya rais mpya, hawafanyi hivyo. Lakini Trump inawezekana kuwa ni rais wa kwanza wa Marekani kuahidi mambo mengi.

Katika hotuba yake wakati mmoja amesema “kila kitu ambacho kimevurugika katika nchi yetu tutaweza kukirekebisha. Kila tatizo linaweza kutatuliwa.”

XS
SM
MD
LG