Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Oktoba 04, 2023 Local time: 16:59

Somaliland iko karibu kutangaza hali ya njaa


Hali ya ukame yaikumba Somaliland

Viongozi wa Somaliland, ambayo imejitenga na Somalia, wanasema kuna hali ya njaa katika maeneo yao wakati serikali hiyo imesimamisha programu za maendeleo kutokana na kuendelea kwa ukame ambao umewauwa dazeni ya watu na karibu mifugo yote imeangamia katika upande wa mashariki wa eneo hilo.

Akizungumza na VOA huko Hargeisa, Somaliland makamu wa rais Abdirahman Abdullahi Seylici amesema hali ya ukame inaonyesha kuwa itazidi kuwa mbaya katika sehemu za mashariki ya nchi hiyo na kuongezeka kwa hatari ya njaa.

Seylici amesema “Sisi tunaikaribia njaa, tathmini tuliofanya na ile iliyofanywa na mashirika ya misaada inaonyesha njaa iko karibu kutangazwa upande wa mashariki ya eneo la Somaliland, kwa sababu hali ya msimu wa mvua hivi sasa haujaanza na kuna uhaba mkubwa wa maji na watu wanapoteza mifugo yao."

Seylici amesema wana chakula na fedha kidogo katika kukabiliana na ukame na uchumi umeathirika vibaya sana kutokana na ukame.

Amesema wameamua kusitisha programu za maendeleo kwa ajili ya kudhibiti bajeti yao ili wawe tayari kukabiliana na balaa la ukame pindi hali itapokuwa mbaya zaidi.

“Pale kulipokuwa na wasiwasi kuwa watu wengi wanaweza kufa kwa sababu ya hali ya ukame kuendelea kuwa mbaya zaidi, tuliamua kusitisha kujenga miradi ya maendeleo. Bajeti yetu imeathirika kutokana na ukame na pia kutokana na Saudi Arabia kupiga marufuku uingizaji wa mifugo kutoka Somaliland,” amesema Makamu wa Rais wa Somaliland.

“Kwa hivyo tumeamua kuelekeza fedha zote katika mambo ya dharura, kwa ajili ya kuokoa watu wasife na misaada ya ukame inayohitajika,” ameongeza kusema.

Huko Somaliland, jamii za wafugaji katika maeneo yote ya eneo hilo wamesema hawajawahi kuona hali mbaya kama hii ya ukame.

Makamu wa rais Somaliland Abdirahman Abdullahi Seylici ameiambia VOA kuwa anaweza kuthibitisha vifo vya watu 10 ambao wamekufa kwa njaa katika nchi yote ya Somaliland, idadi ambayo ni ndogo kuliko ile iliyotolewa kabla ya hapo na maafisa wengine wa Somaliland.

Shirika la Unicef limesema Ijumaa kuwa watoto wengi zaidi wanakabiliwa na hatari wakati Somalia imekumbwa na ukame na balaa la njaa kubwa mno.

Kuna ripoti kuwa mikoa ya mashariki ya Somaliland imekumbwa na kipindipindu kwa kuwa watu waliofikiwa na ukame wamelazimika kunywa maji machafu katika visima vilivyokauka.

UN inasema kuwa zaidi ya Wasomali milioni 6 wanahitaji msaada wa dharura wa chakula, wakiwemo takriban watoto milioni moja ambao wameathirika vibaya sana na utapiamlo.

XS
SM
MD
LG