Maafisa wa Somalia wanasema Fazul Abdullah Mohammed, anayeaminika kuwa kiongozi wa kundi la al-Qaida Afrika Mashariki ameuwa baada ya mashambulizi na polisi.
Fazul Mohammed inaaminika alikuwa mshiriki mkubwa katika mashambulizi ya mabomu ya mwaka 1998 katika balozi za Marekani huko Dar es Salaam na Nairobi. Marekani ilikuwa inamchukulia Fazul kama gaidi anayetafutwa sana duniani na ilitangaza zawadi ya dolla millioni tano kwa maelezo yatakayosababishwa kukamatwa kwake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton, akiwa nchini Tanzania Jumamosi, alisema kifo cha Fazul Mohammed ni "pigo kubwa kwa al-Qaida" na "mwisho halali" kwa mtu aliyehusika katika mauaji ya watu wengi wasio na hatia.
Maafisa nchini Somalia walisema Jumamosi kuwa Fazul Mohammed na mtuhumiwa mwingine wa ugaida waliuawa na polisi siku kadha zilizopita katika kizuizi cha barabarani karibu na Mogadishu. Tangazo la vifo hivyo lilicheleweshwa mpaka utambulisho wao uweze kuthibitishwa, hatua ambayo maafisa wanasema waliifanikisha kwa kulinganisha picha na maiti hizo. Shirika la habari la Ufaransa AFP linasema vipimo vya DNA pia vilifanyika.
Polisi wanasema Fazul ambaye alikuwa akitumia majina kadha ya bandia alikuwa amebeba maelfu ya dolla na vitambulisho kadha ikiwa ni pamoja na passport ya Afrika Kusini.