Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Septemba 26, 2022 Local time: 13:14

Ethiopia yakamata wanaharakati wa upinzani


Ramani ya eneo la Oromia Ethiopia

Ethiopia imewakamata dazeni ya wanaharakati wa upinzani ikisema ni juhudi zinazolenga kuzuia maandamano ya umma kama yale yanayoshuhudiwa kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati.

Mwandishi wa VOA Peter Heinlein anaripoti kutoka Addis Ababa kuwa watu wengi wanaokamatwa ni wale wa jimbo lenye mzozo wa kisiasa la Oromia.

Viongozi wa upinzani kutoka jamii ya Oromo wanasema zaidi ya wanachama wake mia moja wamekamatwa na maafisa wa serikali katika muda wa wiki mbili zilizopita.

Wanasema wengi wa waliokamatwa wanashtakiwa kwa makosa madogo madogo ikiwemo kubishana na majirani zao.

Bekele Gerba naibu mwenyekiti wa kundi la Oromo Federalist Movement anasema ukamataji huo umezusha hofu miongoni mwa wanaharakati wa upinzani katika eneo kubwa la Ethiopia.

Anasema yeyote anayezungumza lugha ya Oromia na ambaye si mwanachama wa chama tawala ni mtuhumiwa na anaweza kukamatwa na kufungwa jela wakati wowote, na kwa hiyo watu wengi wana khofu.

Lakini viongozi wa eneo hilo la Oromia walioko kwenye serikali wamekanusha kuwa kuna nia yoyote ya kisiasa inayohusiana na kukamatwa kwa wanaharakati hao. Msemaji Mesfin Assefa anasema serikali inaheshimu haki za kisiasa za wapinzani, na kwamba kuna kanuni za kisheria nchini humo. Anasema yeyote anayekiuka sheria atawajibishwa kulingana na makosa yake.

Kukamatwa kwa wanaharakati wa upinzani nchini Ethiopia kumetokea wakati maafisa wa serikali wanakiri kuwa wana wasiwasi juu ya msukosuko wa kisiasa katika ukanda huo.

Waziri mkuu Meles Zenawi mwezi huu amesema kuwa ana wasiwasi kuhusu kuyumbayumba kwa hali ya kisiasa nchini Yemen, nchi iliyo umbali wa kilomita 150 kutoka mpaka wa kaskazini wa Ethiopia. Meles alisema baadhi ya makundi ya upinzani yanajaribu kuiga msukosuko huo wa kisiasa.

XS
SM
MD
LG