Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 18, 2024 Local time: 21:56

Ethiopia yabadili msimamo kuelekea Eritrea


Waziri mkuu wa Ethopia Meles Zenawi akihutubia mkutano mlkuu wa Umoja wa Mataifa.
Waziri mkuu wa Ethopia Meles Zenawi akihutubia mkutano mlkuu wa Umoja wa Mataifa.

Serikali ya Ethiopia imetangaza mabadiliko katika sera zake za kigeni kwa lengo la kuitimua madarakani serikali jirani ya Eritrea.

Katika mfululizo wa mahojiano wiki iliyopita, maafisa wa Ethiopia wameeleza mabadiliko ya sera yao kuhusu Eritrea kutoka kwenye dhana ya kujikinga, kuelekea kwenye hatua za kuiondoa serikali ya Asmara.

Vyombo vya habari vilimnukuu Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi akizungumza na kituo cha redio cha upinzani nchini Eritrea kuwa serikali yake itafanya kazi katika misingi ya kidiplomasia na kijeshi kuuondoa utawala wa Rais Isaias Afewerki. Taarifa hizo hazikutoa maelezo zaidi.

Awali, serikali ya Ethiopia iliwashutumu wapinzani wake kwa kupeleka kundi la washukiwa wa ugaidi huko Addis Ababa mwezi Januari ili kuvuruga amani katika mkutano uliomalizika hivi karibuni wa Umoja wa Afrika. Maafisa wanasema washukiwa hao wakiwa wamebeba milipuko walikamatwa na mpango wao kuharibiwa.

Msemaji wa serikali ya Ethiopia hakutoa maelezo ya ziada kuhusu kukamatwa huko alipozungumza Jumapili.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Meles Zenawi, alilieleza waandishi wa habari kuwa serikali yake imegundua ushahidi kwamba Eritrea inajaribu kuwezesha mapinduzi kama ya kaskazini mwa Afrika nchini Ethiopia.

Katika mahojiano na VOA hapo Jumapili, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia, Dina Mufti amesema uamuzi wa kuweka msimamo mkali dhidi ya Eritrea ulifikiwa baada ya jumuiya ya kimataifa kuonekana kutosikia kilio chao cha kuweka shinikizo zaidi kwa Eritrea.

Dina amesema Ethiopia imelazimishwa kuchukua kile alichoita “hatua muhimu” kwa sababu tishio kutoka Eritrea limeongezeka.

Eritrea ilijitenga kutoka Ethiopia na kupata uhuru wake mwanzoni mwa miaka ya 1990 baada ya miaka 30 ya kuuhangaikia. Meles Zenawi na Rais wa sasa wa Eritrea Isaias Afewerki, walikuwa washirika katika harakati za uhuru, lakini baadaye uhusiano baina yao uliharibika, na kusababisha miaka miwili ya vita vya mpakani kati ya mwaka 1998 na 2000 ambavyo viliua watu wapatao 70,000.

Juhudi za VOA kuwasiliana na wasemaji wa Eritrea kwa njia ya simu kutoa maoni kuhusu tuhuma hizo zilishindikana, lakini serikali hiyo imepinga vikali mpango wowote wa kuidhoofisha Ethiopia.


XS
SM
MD
LG