Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 26, 2023 Local time: 05:19

ECOWAS inakabiliwa na mtihani mgumu katika ukanda wa Afrika Magharibi - Wachambuzi


PICHA YA MAKTABA: Mkutano wa kamati ya ECOWAS mjini Accra, Ghana

Msururu wa mapinduzi katika ukanda wa Afrika Magharibi unaweka umoja na uwezo wa jumuiya ya kikanda ya ECOWAS, katika mtihani, huku ikijaribu kurejesha utawala wa kiraia katika nchi kama vile Burkina Faso, Guinea, Mali na Niger.

Mataifa hayo manne yameungana kupinga vikwazo vya kiuchumi, na hatua zinazoweza kuchukuliwa za kijeshi, na nchi zingine 11 wanachama wa jumuiya hiyo. Wataalam wanaonya uwezo wa ECOWAS kushughulikia changamoto za kiusalama unahatarishwa na kuongezeka kwa viongozi wapya wa kijeshi.

Jumuiya hiyo ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi inatatizika jinsi ya kukabiliana na utawala wa kijeshi nchini Niger, ambao umekuwa madarakani kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Mnamo Julai 26, wanajeshi walimweka Rais Mohamed Bazoum katika kizuizi cha nyumbani, wakishutumu utawala wake kwa kusimamia vibaya rasilimali za nchi na kuruhusu hali ya usalama kuzorota. Kwa kujibu, ECOWAS iliiwekea Niger vikwazo vya kibiashara na hata kutishia kuingilia kijeshi.

Rais aliyeondolewa wa Niger Mohamed Bazoum alipokuwa Berlin Ujerumani, Julai 8, 2021. Picha na Bernd von Jutrczenka/Pool kupitia REUTERS.
Rais aliyeondolewa wa Niger Mohamed Bazoum alipokuwa Berlin Ujerumani, Julai 8, 2021. Picha na Bernd von Jutrczenka/Pool kupitia REUTERS.

Lakini mizozo ya kisiasa na kiusalama inayoendelea nchini Niger, Burkina Faso, Guinea, na Mali inaonekana kuwa changamoto kwa nchi nyingine 11 wanachama wa ECOWAS.

Paul Melly, mshauri wa masuala ya Afrika katika taasisi ya Chatham House, mjini London, anasema viongozi wa mapinduzi hawazingatii masharti yaliyowekwa na ushirikiano wa jumuiya hiyo ya kikanda.

"Msururu huu wa mapinduzi, ni pigo kubwa sana kwa kile kilichokuwa nguvu kuu ya ECOWAS. Na ukweli kwamba tawala za kijeshi zinakaidi utamaduni wa muda mrefu wa ECOWAS wa kushirikiana katika kuweka kanuni za utawala, na katika kudhibiti mizozo ni tishio la kweli, na ni changamoto kwa umoja wa kikanda, " anasema.

Mnamo mwaka wa 2017, ECOWAS ilisifiwa kwa hatua yake ya kijeshi ya pamoja dhidi ya Rais wa Gambia Yahya Jammeh, na kumlazimisha kujiuzulu baada ya kushindwa katika uchaguzi wa rais wa sasa, Adama Barrow.

Waandamanaji nchini Niger.
Waandamanaji nchini Niger.

Francis Mangeni, mtaalam wa utangamano wa kikanda, anabainisha kuwa hali ya sasa ni tofauti kabisa, huku baadhi ya mapinduzi yakiungwa mkono na wananchi.

"Sasa tuko katika hali ambayo haiko wazi, ambapo watu wenyewe wanaunga mkono mapinduzi. Kwa hiyo hii inaleta aina fulani cha changamoto. Kwa hiyo, kwa maneno mengine, uhalali wa serikali iliyochaguliwa kikatiba unaonekana kuwa katika shaka. Na hili ni jambo la ajabu kusema, kwa sababu, ikiwa serikalia ni za kikatiba, zinapaswa kuwa halali, lakini inaonekana watu hawafikiri hivyo," anasema.

Viongozi wa Umoja wa Afrika wamekuwa wepesi kuwashutumu wakuu wa nchi wanaobadilisha katiba ili kuongeza muda wao wa kukaa madarakani na kubadilisha ukomo wa umri ili kubaki madarakani.

Kulingana na wataalamu hao, kuongezeka kwa utekaji wa kijeshi barani Afrika kunatokana na viongozi kukatalia kwenye madaraka, dosari katika uchaguzi, na viongozi waliochaguliwa kushindwa kufanya kazi kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi. Kwa kufahamu changamoto hizo, Seneti ya Nigeria ilimshauri Rais Bola Tinubu, ambaye pia anaongoza ECOWAS, kutafuta mbinu mbadala za kushughulikia mgogoro wa Niger.

Melly anasema kuwa nchi zilizoathiriwa za mapinduzi sasa zinachukulia migogoro yao kama masuala ya ndani.

"Utamaduni wa ushirikiano ambao kimsingi nchi zote za ECOWAS zilikubali kwamba utatuzi wa matatizo ya ndani ya nchi wanachama lilikuwa ni jukumu la jumuiya nzima, umedhoofika kwa kiasi kikubwa, kwa sababu hazikubaliani na dhana hiyo, kwamba ECOWAS kwa ujumla wake ina haki ya kuhusika katika kusimamia migogoro yao na kurejesha nchi kwenye utawala wa kikatiba. Na hayo ni mabadiliko makubwa sana," alisema Melly.

Wachambuzi wanasema eneo hilo linahitaji kuungwa mkono na mataifa mengine ya Afrika ili kutatua matatizo ya mapinduzi ya mara kwa mara na majaribio ya mapinduzi.

Umoja wa Afrika tayari umezisimamisha uanachama wa nchi sita ambapo vikosi vya kijeshi vilinyakua mamlaka kutoka kwa raia, zikiwemo nchi nne za ECOWAS, Gabon na Sudan.

Forum

XS
SM
MD
LG