Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 26, 2024 Local time: 11:48

Ebola imeua watu 29 Uganda, na WHO inasema chanjo ipo tayari kufanyiwa majaribio


Maafisa wa afya wakiwa nje ya kituo maalum kwa ajili ya wagonjwa wa Ebola katika hospitali ya rufaa ya Mubende, Uganda. Sept 29 2022. PICHA: AP
Maafisa wa afya wakiwa nje ya kituo maalum kwa ajili ya wagonjwa wa Ebola katika hospitali ya rufaa ya Mubende, Uganda. Sept 29 2022. PICHA: AP

Watu 29 wamefariki kutokana na mlipuko wa virusi vya Ebola nchini Uganda. Maafisa wa afya 4 ni miongoni mwa waliofariki.

Watu 63 wamewekwa chini ya uangalizi wa maafisa wa afya baada ya kuonyesha dalili za maambukizi

Maafisa wa afya 10 wameambukizwa virusi vya Ebola.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kwamba chanjo inayotumika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Ebola katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haiwezi kutumika dhidi ya virusi vya Ebola Uganda.

Vifo vya madaktari vinaongezeka

Wairi wa Afya wa Uganda Jane Ruth Achieng, ameandika ujumbe wa Twitter kwamba Margaret Nasisubi, afisa wa afya, anakuwa wa nne kufariki kutokana na Ebola. Daktari raia wa Tanzania alikuwa afisa wa kwanza wa afya kufariki duniani kutokana na Ebola nchini Uganda.

Tedros amesema kwamba “kuna aina mbalimbali za chanjo ambazo zinaendelea kutengenezwa na mbili kati ya hizo zinasubiri kufanyiwa majaribio katika wiki za hivi karibuni nchini Uganda endapo serikali ya Uganda itaruhusu majaribio hayo.”

Shirika la Afya Duniani limesema kwamba linaisaidia Uganda kukabiliana na maambukizi ya Ebola, ambayo yameripotiwa katika wilaya nne.

Kisa cha kwanza cha maambukizi kiliripotiwa katika wilaya ya Mubende kabla ya kugunduliwa katika wilaya za Kassanda, Kyegegwe na Kagadi.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kwamba hatatoa amri ya kusitisha shughuli za kawaida na watu kubaki nyumbani kama hatua ya kudhibithi maambukizi ya virusi vya Ebola, akisisitiza kwamba “hakuna haja ya watu kuwa na wasiwasi.”

Mlipuko wa Ebola Uganda ni tofauti na wa DRC

Virusi vya Ebola viligunduliwa mwaka 1976 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Uganda inakabiliana na aina ya Ebola kutoka Sudan ambayo ni tofauti ya Ebola ya DRC.

Uganda ni jirani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo imeripoti milipuko kadhaa ya Ebola. Watu 5 wamefariki DRC mwaka 2019 katika mlipuko wa hivi karibuni.

DRC iliripoti kumalizika kabisa kwa maambukizi ya Ebola mwezi uliopita. Watu 2,280 walifariki DRC mwaka 2020 kutokana na Ebola.

Zaidi ya watu 11,300 walifariki duniani kati ya mwaka 2013 na 2016 Afrika Magharibi kutokana na maambukizi ya virusi vya Ebola.

Dalili za maambukizi ya Ebola

Dalili za maambukizi ya ebola ni pamoja na joto jingi mwilini, mgonjwa kutapika, kutokwa damu na kuharisha. Mara nyingi ni vigumu kuzuia maambukizi hasa mijini kwenye idadi kubwa ya watu.

Watu walioambukizwa Ebola, hawaonyeshi dalili hadi baada ya siku 21.

Hakuna tiba ya Ebola kufikia leo japo utafiti unaendelea kutafuta tiba hiyo.

XS
SM
MD
LG