Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 10, 2022 Local time: 12:40

Chadema yaonya wanaotaka kuvuruga uchaguzi Tanzania


Mgombea urais wa Chadema Tundu Lissu

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema kimesema kitaendesha siasa zake kwa amani na kuonya kwamba yeyote atayejaribu kuvuruga uchaguzi huo atawajibika. 

Kauli ya chama hicho inakuja huku vyombo vya dola nchini humo vikionya kuanza kutumia nguvu dhidi ya wanasiasa watakao onekana kukiuka sheria za uchaguzi na utoaji wa lugha za uchochezi.

Chama hicho ambacho mgombea wake, Tundi Lissu yuko Mkoani Kilimanjaro katika moja ya ngome zake akiendelea na kampeni, kimesema kinaamini kitafanya uchaguzi wa amani na kwamba hakitakuwa tayari kuona haki yake inapokonywa.

Bila kutaja mamlaka yoyote wala chombo chochote, kimesema iwapo kutajitokeza na mtu yoyote atahusika kutibuwa ama kuvuruga uchaguzi huo basi atawajibika moja kwa moja. Hata hivyo hakikusema atawajibika kwa namna gani.

Katika hatua nyingine, baraza la wazee la chama hicho limebainisha namna kitakavyoweka mkazo wa kuwajali wazee iwapo kitafanikiwa kuchukua dola katika uchaguzi wa Oktoba 28.

Akitoa ujumbe wa chama katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani yaliyoadhimishwa Alhamisi, Katibu Mkuu baraza la wazee Bazecha, Rodelik Lutembeka amedai ustawi wa wazee wengi nchini bado uko nchini kama vile kupuuzwa kulipwa mafao yao baada ya kustaafu kazi.

Wakati chama hichi kikitoa msimamo huo, vumbi la kampeni kuelekea kilele cha uchaguzi limeendelea kutimuka huku wagombea wa chama tawala CCM na Chadema wameendelea kupishana kanda na kila mmoja akiahidi kuipeleka mbele Tanzania.

Tundu Lissu
Tundu Lissu

Lissu anayewania nafasi ya urais kwa mara ya kwanza kutoka chama kikuu cha upinzani ameanza leo kampeni zake katika majimbo ya mkoa wa Kilimanjaro, eneo ambalo chama hicho kimekuwa kikijivunia kufanya vyema katika chaguzi mbalimbali.

Mgombea wa CCM, Rais John Magufuli Alhamisi amenadi sera zake katika mkoa wa Songwe na kufika hadi Tunduma eneo liliko mpakani na Zambia.

Huku wagombea wao wakiendelea kusaka kura kwa wananchi, tume ya taifa ya uchaguzi NEC imeonya juu ya mwenendo wa kuwarubuni wapiga kura kwa kuchukua kadi zao.

Mgombea urais wa CCM John Pombe Magufuli
Mgombea urais wa CCM John Pombe Magufuli

Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage amesema kitendo chochote cha kuchukua kadi ya mpiga kura kwa njia ya kilaghai ni kinyume cha sheria.

Katika hatua nyingine, Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa mwishoni mwa wiki imepanga kukutana na viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu kwa ajili ya kujadiliana yale yanayoendelea kwenye kampeni.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, George Njogopa, Tanzania

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG