Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 06:37

HRW yasema Tanzania yakandamiza uhuru kuelekea uchaguzi mkuu


Rais Magufuli akizindua kampeni yake ya uchaguzi Tanzania, August 29, 2020
Rais Magufuli akizindua kampeni yake ya uchaguzi Tanzania, August 29, 2020

Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dr. Hassan Abbas, ajibu kuwa madai hayo hayana msingi wowote na hayana budi kupuuzwa.

Shirika la kutetea haki za Binadamu -Human Rights Watch – limeishutumu serikali ya Tanzania kwa kile ilichosema ni ukandamizaji wa wanasiasa wa upinzani, vyombo vya habari, na mashirika yasiyo ya kiserikali kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu.

Katika ripoti yake mpya iliyotolewa Jumatano mjini Nairobi, Kenya, HRW imesema serikali ya Tanzania imeendelea kuwakamata wanasiasa wa upinzani, ikisema kuna wanasiasa wa upinzania na wakosoaji wa serikali 17 ambao wamekamatwa kuanzia mwezi Juni.

Serikali ya Tanzania mara moja imejibu tuhuma hizo ikisema, kupitia Msemaji Mkuu wa Serikali, Dr. Hassan Abbas, kuwa madai hayo hayana msingi wowote na hayana budi kupuuzwa.

“Haya madai ni ya kuungaunga, Tanzania inaheshimu uhuru wa habari na ndio maana tuna redio 183 ziko hewani hivi tunavyozungumza, magazeti zaidi ya 240 na TV zaidi ya 40 na itaendelea kuheshimu uhuru huo,” alisema Dr. Abbas.

Katika ripoti hiyo HRW imesema mashirika kadhaa ya kutetea haki za kibinadamu yamepigwa marufuku na leseni zao kufutwa huku makundi kadhaa ya kufuatilia uchaguzi yakiwa yamenyimwa kibali cha kufuatilia uchaguzi mkuu ujao.

Ripoti hiyo imeendelea kusema vyombo vya habari vimeekewa masharti makali, baadhi vikifungiwa na leseni zao kufutwa hasa vinaporipoti kuhusu janga la virusi vya Corona nchini Tanzania. Rais John Magufuli amesisitiza kwamba virusi vya Corona havipo kabisa nchini humo.

“Ni wazi kwamba serikali ya Tanzania imeongeza vitendo vya kukandamiza upinzani, wanaharakati na vyombo vya habari kuelekea uchaguzi mkuu,” amesema mkuu wa utafiti wa HRW Afrika, Oryem Nyeko, akiongezea kwamba “badala ya kuweka mazingira bora ya kuhakikisha kwamba watu wake wana haki ya kujieleza wakati huu, maafisa wa serikali wameamua kuchukua hatua ambazo zinaleta mazingira ya kutilia shaka iwapo uchaguzi mkuu utakuwa huru na haki.”

Ripoti hiyo inaendelea kusema kwamba serikali ya Tanzania imeendelea kuwakamata na kuwazuilia wanasiasa wa upinzani, hasa wa vyama vya vikuu vya upinzani, ACT–Wazalendo na Chadema.

HRW imetoa mfano wa kukamatwa kwa kiongozi wa kiislamu Issa Ponda, mnamo mwezi July, ambaye alizuiliwa kwa muda wa siku tisa baada ya kufanya kikao na waandishi wa habari akitaka serikali kuandaa uchaguzi mkuu ulio huru na haki.

Tanzania Yajibu

Serikali ya Tanzania ilijibu haraka madai hayo Jumatano kupitia Msemaji Mkuu wa Serikali, Dr. Abbas ambaye aliambia VOA kwamba waandishi wa ripoti hiyo hawakutoa nafasi kwa serikali ya Tanzania kujibu tuhuma hizo.

Dr. Abbas aliongeza kuwa “ni vyema wanaharakati wakathamini hatua zinazochukuiwa na Serikali katika kudhibiti makosa ya uandishi wa habari kwani wako wanahabari wanaokosea sana, isichukuliwe kila sheria inayotungwa eti imebana uhuru.”

Aliendea kusema “kwa mfano hizo Kanuni mpya za Mitandaoni zinazuia kusambaza picha za vitendo vya ngono. Watu walitaka nchi hii ijae picha za uchi?”

Abbas alimalizia kwa kusema masharti hayo yalikuwa muhimu na yalikuwa katika viwango vya kimataifa.

XS
SM
MD
LG