Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Juni 22, 2024 Local time: 15:49

Bola Tinubu ameshinda urais Nigeria, wapinzani wanataka uchaguzi kurudiwa


Rais mteule wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu (katikati) alipowasili katika kito cha kupiga kura, Ikeja, Lagos, Nigeria. Feb 25, 2023
Rais mteule wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu (katikati) alipowasili katika kito cha kupiga kura, Ikeja, Lagos, Nigeria. Feb 25, 2023

Bola Ahmed Tinubu ametangazwa mshindi wa kura za urais nchini Nigeria katika uchaguzi ambao wagombea wengine wameyakataa matokeo hayo wakisema umejaa udanganyifu na kutaka urudiwe.

Tinubu, mwenye umri wa miaka 70, amepata asilimia 37 ya kura, ikiwa ni karibu kura milioni 8.8 huku mshindani wake wa karibu Atiku Abubakar amepata asilimia 29, sawa na kura milioni 7 na Peter Obi akamaliza katika nafasi ya tatu akiwa na asilimia 25.

Bola Tinubu, mgombea wa chama tawala cha All progressive congress APC, ametangazwa mshindi mapema jumatano, huku wagombea wengine wawili katika kinyang’anyiro cha urais wakitaka upigaji urudiwe.

Kuna ripoti kwamba wapinzani wa Tinubu – Atiku Abubakar na Peter Obi, wanatarajiwa kupinga matokeo hayo mahakamani.

Abubakar alimaliza katika nafasi ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2019, kesi yake aliyowasilisha mahakamani kupinga matokeo ilitupiliwa mbali.

Madai ya wizi wa kura

Chama cha rais Mteule Bola Tinubu, cha All progressive congress kimewasihi wagombea wa upinzani kukubali kushindwa na kutosababisha vurugu katika nchi hiyo yenye idadi kubwa ya watu Afrika.

Wagombea wa upinzani wanasema kwamba udanganyifu katika hesabu ya kura ulifanyika wakati wa kuchapisha matokeo.

“Changamoto zilizoripotiwa zilikuwa chache sana na haziwezi kubadilsha matokeo ya jumla. Tuwe wakweli kuhusu uhalisia wa matokeo na hesabu kamili inasema hivyo. Na ndivyo jumuiya ya kimataifa inavyosema,” amesema rais mteule wa Nigeria Bona Tinubu.

Tinubu amekuwa mwenye ushawishi mkubwa katika siasa za Nigeria bila kuwa mstari wa mbele, kwa muda mrefu ambao amekuwa katika siasa amechukuliwa kama nguzo muhimu katika siasa za Nigeria, ambaye amekuwa akiidhinisha wagombea katika nafasi mbalimbali.

Ushawishi wa Tinubu ulimsaidia rais anayeondoka Muhammadu Buhari kushinda mihula miwili madarakani, katika uchaguzi wa mwaka 2015 na 2019.

Tangu alipoacha ugavana wa Lagos mwaka 2007, Tinubu amekuwa akiidhinisha wagombea ambao wamekuwa wakishinda ugavana katika mji huo mkubwa Afrika.

Sasa, ana jukumu la kuiongoza Nigeria kutoka katika migogoro na kuboresha rekodi ya Muhammadu Buhari.

“Nchi ni ile ile lakini kulingana na mimi, kinachoweza kufanyika katika nchi nyingine kinaweza kufanyika hapa. Naahidi kwamba nitafanya kazi nanyi ili kuifanya Nigeria kuwa kivutio cha maendeleo na tutashirikiana kuijenga nchi yetu,” amesema Tinubu.

Wafuasi wa Tinubu wafurahia, wa upinzani wamekerwa

Wafuasi wa Tinubu wanasema ni mchapa kazi mwenye rekodi ya kuchagua watu wenye uwezo mkubwa wa kuleta maendeleo. Baba Tunde ni mfanyabiashara mjini Lagos.

“Nina furaha sana. Nilmipigia kura Tinubu ambaye amekuwa rais. Nina matumaini kwamba ataleta mabadiliko. Nilikuwa na ndoto kwamba atakuwa rais na ndoto yangu imetimia.”

“Ni mtu mzuri hapa Nigeria, ni mtu mashuhuri Lagos, amekuwa akiiongoza Lagos kwa miaka mingi na amefaulu. Tulifurahia sana utawala wake Lagos. Tunafuraha kwamba amepanda ngazi na kuongoza serikali kuu. Amefikia kilele, amefanikiwa,” amesema Mushafiy Abina, mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 72.

Wakosoaji wa Tibunu wanasema kwamba huwa anatoa zabuni na kuajiri marafiki zake, na amekuwa na makundi ambayo yanadhibithi mji wa Lagos na kutishia wafuasi wake iwapo hapati anayotaka. Sylvia Mmesoma, ni mwanafunzi.

“Hata sina la kusema. Kwanini Tinubu? Nimeona wakitangaza matokeo na nimekataa kukubali. Sisi raia wa Nigeria tumekataa kukubali matokeo hayo kwa sababu wizi umefanyika kwa hivyo tunastahili kufanya lolote linalowezekana kuhakikisha kwamba rais anayestahiki anashinda.”

Peter Obi aliwashitua raia wengi wa Niageria aliposhinda Lagos, jimbo lenye idadi kubwa ya wapiga kura na ngome ya muda mrefu ya Tinubu.

Obi alitumia mitandao ya kijamii na kuwafikia wapiga kura moja kwa moja katika kampeni zake. Aliwavutia wapiga kura kwa ahadi kwamba watabadilisha mfumo wa siasa wa Nigeria.

Nigeria inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa usalama.

XS
SM
MD
LG