White House ilisema kuwa Biden alikuwa akifuata itifaki kwa kutompigia simu na kumpongeza rasmi Sunak, ambaye ana asili ya India, na ambaye babake alizaliwa Kenya na mamake Tanganyika, hadi atakapokutana na Mfalme Charles III siku ya Jumanne kupata idhini ya kuunda serikali.
Sunak, alipata uungwaji mkono na wabunge wa Chama cha Conservative, kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo, kufuatia kujiuzulu kwa Liz Truss wiki iliyopita, ambaye alikuwa katika afisi hiyo kwa chini ya miezi miwili.
Sunak atakuwa waziri mkuu wa tatu wa Uingereza katika muda wa wiki saba tu, baada ya kipindi cha machafuko ya kisiasa ambayo yameharibu taswira ya kimataifa ya nchi hiyo. Huku mfumuko wa bei ukiwa zaidi ya 10% na uchumi ukitabiriwa kudorora, huenda tafrija ya kisiasa ya Sunak itakuwa fupi.
Sunak alitoa hotuba fupi ya televisheni Jumatatu kutoka makao makuu ya Chama cha Conservative huko London.
"Uingereza ni nchi nzuri mno, lakini hapana shaka tunakabiliwa na changamoto kubwa ya kiuchumi. Sasa tunahitaji utulivu na umoja,” alisema.
"Kitakuwa kipaumbele changu kikubwa kuleta chama chetu na nchi yetu kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kushinda changamoto zinazotukabili na kujenga mustakabali bora na wenye mafanikio," aliongeza.
Sunak anatarajiwa kumtembelea Mfalme Charles III Jumanne kukubali mwaliko wa kuunda serikali.