Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Mei 20, 2024 Local time: 14:37

Amnesty international wanataka Tanzania kufuta sheria zote kandamizi zilizotungwa kwa amri ya rais


Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan (kulia), akiwa katika mkutano na kiongozi wa upinzani Tundu Lissu ambaye anaishi uhamishoni Brussels, Ubelgiji. Feb 16, 2022
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan (kulia), akiwa katika mkutano na kiongozi wa upinzani Tundu Lissu ambaye anaishi uhamishoni Brussels, Ubelgiji. Feb 16, 2022

Shirika la amnesty international linataka serikali ya Tanzania kufuta sheria zote zilizoundwa kutokana na kile imetaja kama amri ya rais na ambazo raia wa Tanzania wanaziona kama sheria kandamizi.

Kati ya sheria hizo ni zinazohusiana na ugaidi na uhalifu wa kiuchumi.

Shirika la amnesty international linataka sheria hizo kufutwa baada ya rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuondoa marufuku dhidi ya shughuli za vyama vya upinzani iliyowekwa mwaka 2017 wakati wa utawala wa Hayati John Magufuli.

Amnesty international imetaja hatua hiyo kuwa nzuri lakini kwamba juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha kwamba hali za raia wa Tanzania zinalindwa.

Roland Ebole, mtafiti wa Amnesty international Afrika mashariki na kati, amesema katika mahojiano na Sauti ya Amerika kwamba serikali ya Tanzania inastahili kufanyia marekebisho au kuondoa kabisa sheria ya sasa inayosimamia vyama vya kisiasa ili kuondoa vizuizi vyote vya uhuru wa kujieleza, kukusanyika, na kuandamana kwa amani.

“Mabadiliko lazima yaanze kuondoa sheria zote zilizotungwa kutokana na amri ya rais wakati wa utawala wa John Magufuli. Serikali ya Tanzania inastahili kuongozwa na sheria na wala sio amri za rais au kiongozi aliye madarakani,” amesema Roland.

Amri ya kusitisha shughuli za vyama vya upinzani Tanzania

Aliyekuwa rais wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli alitangaza amri ya kusitisha shughuli zote za vyama vya kisiasa mwaka 2016.

Polisi walizuia na kuwakamata wanasiasa wa upinzani akiwemo kiongozi wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEM, Freeman Mbowe aliyezuiliwa kwa karibu miezi 8, baada ya kufunguliwa mashtaka ya ugaidi kwa kufanya mkutano wa kisiasa.

Alidaiwa kwamba alikuwa anapanga kulipua vituo vya mafuta. Wanasiasa wa chama kinachotawala cha mapinduzi CCM hata hivyo walikuwa huru kufanya mikutano.

Mbowe aliachiliwa baada ya shinkizo za ndani na nje ya Tanzania na mazungumzo yamekuwa yakiendelea kati ya vyama vya upinzani na rais Samia Suluhu Hassan.

Amnesty international wansema kwamba raia Samia anaonekana kutaka kubadilisha sera kandamizi nchini Tanzania kwa kujijengea sifa kama kiongozi mwema, ikiwemo kuweka uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.

Lakini linaonya kwamba huenda pakatokea kiongozi mwingine atakayeharibu yote anayofanya rais Samia na kuirejesha Tanzania katika sera kandamizi na hivyo kutaka bunge kutekeleza wajibu wake wa kutunga sheria na wala sio kuongozwa kwa amri za rais.

“Sheria hazifai kutungwa na amri za rais wakati wowote anapojisikia kwamba ni vyema kufanya hivyo au kwa hiari yake. Bunge ndilo linafaa kutunga sheria. Rais mwingine akiingia madarakani, anaweza kutunga sheria zake pasipo kuzingatia sheria zilizopo na vyombo vya serikali kutumia amri hizo kama sheria,” ameendelea kusema Roland Ebole, afisa wa Amnesty international.

Katiba mpya Tanzania kupunguza mamalaka ya rais

Mchakato wa kuandika katiba mpya Tanzania ulioanzishwa na aliyekuwa rais Jakaya Kikwete haukuendelezwa na utawala wa hayati John Magufuli.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema yupo tayari kuanza majadiliano kuhusu kuandikwa kwa katiba mpya.

Miongoni mwa maswala makubwa yanayojadiliwa ni kupunguza madaraka ya rais.

XS
SM
MD
LG