Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Aprili 24, 2024 Local time: 12:44

Watu 13 wapoteza maisha, 6 kujeruhiwa katika ajali nchini Uganda


Ramani ya Afrika Mashariki
Ramani ya Afrika Mashariki

Polisi nchini Uganda wanasema watu 13, kati yao watanzania 12, wamefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea katika barabara kuu ya Masaka.

Msemaji wa Jeshi la Polisi la Uganda Asan Kasingye aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu kwamba waathirika wengi walikuwa wakisafiri katika basi dogo ambalo liligongana uso kwa uso na lori jumapili usiku. Raia hao wa Tanzania walikuwa wakisafiri kurudi nyumbani wakitoka harusini.

Anasema abiria wengine kwenye basi dogo waliumia vibaya na wako katika hali mahututi. Abiria mmoja kwenye lori alifariki wakati dereva ameumia vibaya. Barabara hiyo magharibi mwa Uganda imekuwa na ajali nyingi katika miaka kadhaa kutokana na ajali nyingi mbaya ambazo zinasababishwa na madereva wasio makini.

Wakati huohuo vyanzo vya habari nchini Tanzania vimesema kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Tanzania, Augustine Ollomi amesema Watanzania hao walikwenda Uganda kwa ajili ya shughuli ya harusi lakini hana taarifa walikwenda sehemu gani nchini humo. Amesema wanaendelea kufanya mawasiliano na mamlaka za Uganda kujua undani wa ajali hiyo.

“Ni kweli tumefuatilia basi hilo na kubaini kwamba liliondoka hapa nchini Septemba 15 kwenda Uganda kwenye shughuli ya harusi. Mengine siwezi kusema zaidi mpaka tutakapofanya mawasiliano na mamlaka za Uganda,” amesema Ollomi.

Majeruhi walipelekwa Hospitali ya Nkozi kwa ajili ya matibabu lakini baadaye walipewa rufaa na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mulago. Maiti zote zilipelekwa Hospitali ya Gombe, Uganda.

XS
SM
MD
LG