Taifa hilo dogo linalotawaliwa kimabavu na linalozalisha mafuta la Afrika ya Kati linaongozwa na Rais Teodoro Obiang, mkuu wa nchi aliyetawala kwa muda mrefu zaidi duniani, ambaye anataka kuongeza miaka yake 43 madarakani.
Wagombea wawili wa upinzani walikuwa wakigombea: Buenaventura Monsuy Asumu, ambaye tayari amegombea katika chaguzi tano zilizopita, na Andrés Esono Ondo, ambaye anagombea kwa mara ya kwanza.
Zaidi ya watu 400,000 walijiandikisha kupiga kura katika nchi hiyo yenye takriban watu milioni 1.5.
Wapinzani wamelalamika kuwa ulitokea udanganyifu na ukiukaji wa sheria kwenye uchaguzi huo.
Obiang aliingia madarakani mnamo mwaka 1979 baada ya kuuangusha utawala wa rais wa kwanza aliyeingia madarakani tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake kutoka kwa Uhispania mnamo mwaka 1968.
Katika uchaguzi uliofanyika hapo Jumapili Obiang anatarajiwa kupata zaidi ya asilimia 95 ya kura, na hivyo kuendelea na muhula wa sita.