Jeshi la Uganda limesema kuwa limekamilisha zoezi la kuwaondoa raia wake waliokuwa wamekwama nchini Sudan ya kusini kutokana na machafuko yanayoendelea katika mji wa Juba.
Brigedia Leopard Kyanda ambaye alikuwa akiongoza zoezi hilo ameliambia jarida la Insider la Uganda kuwa watu elfu thelathini wakiwemo raia wa Kenya, Somalia na Tanzania wameondelewa nchini Sudan ya kusini.
Raia hawa walikuwa wamekusanyika katika mji wa Nisutu Sudani ya kusini na wakachukuliwa na jeshi hilo.
Mapigano mapya kati ya wanajeshi wanaomuunga mkono rais wa Sudani ya kusini Salva Kiir na makamu wake Riek Machar huko Juba yamesababisha vifo vya zaidi ya watu mia tatu huku maelfu wakiwa hawana makazi.
Serikali ya Uganda imesema raia wake kumi na moja wamefariki katika mapigano hayo huku sita kati yao wakiwa wamefariki kwa kushambuliwa na majeshi ya Machar. Raia watano kati ya waliookolewa jana wamefariki kwa ajali ya gari wakiwa njiani kuelekea kwenye eneo la usalama.