Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Mei 18, 2024 Local time: 06:52

Wapalestina wakabiliwa na janga la kibinadamu wakati Israeli ikijiandaa kufanya mashambulizi ya ardhini


Tingatinga likiondoa kifusi huku watu wakikusanyika katika eneo la makazi huko Rafah upande wa kusini mwa Ukanda wa Gaza baada ya Israeli kufanya shambulizi Octoba 15, 2023.
Tingatinga likiondoa kifusi huku watu wakikusanyika katika eneo la makazi huko Rafah upande wa kusini mwa Ukanda wa Gaza baada ya Israeli kufanya shambulizi Octoba 15, 2023.

Marekani inasema kivuko cha mpakani ya Ukanda wa Gaza na Misri kitafunguliwa tena,  lakini muda wa ufunguzi huo haujulikani mpaka sasa.

Umoja wa Mataifa umeonya juu ya hali mbaya ya kibinadamu huko Gaza na Israel imewaambia Wapalestina wanaoishi upande wa kaskazini mwa eneo hilo kuondoka kabla ya operesheni ya kijeshi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, aliyerejea nchini Israeli Jumatatu baada ya ziara katika nchi kadhaa nyingine katika eneo hilo, alisema Marekani inafanya kazi na Misri, Israeli na Umoja wa Mataifa kuhakikisha misaada inaingia Gaza na kuwafikia wenye shida.

Picha iliyotolewa na ofisi ya Kasri ya Mfalme wa Saudi Arabia October 15, 2023, inaonyesha Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akikutana na Prince Mohammed bin Salman, mjini Riyadh.
Picha iliyotolewa na ofisi ya Kasri ya Mfalme wa Saudi Arabia October 15, 2023, inaonyesha Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akikutana na Prince Mohammed bin Salman, mjini Riyadh.

“Katika siku chache zilizopita, nimekwenda Israeli, Jordan, Bahrain, Qatar, UAE, Saudi Arabia, na Misri,” Blinken alisema Jumatatu katika akaunti ya Twitter X.

“Kile nilichosikia kutoka kwa kila mshirika wetu ni maoni yao kuhusu kuzuia vita hivi kuenea, kulinda maisha ya watu wasio na hatia, na kupeleka misaada kwa wale wanaohitaji huko Gaza.”

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu ilisema katika taarifa yake Jumatatu kulikuwa hakuna makubaliano yaliyofikiwa kuhusu kusitisha mapigano ili kuruhusu misaada kuingia Gaza na kuwaruhusu wageni kuondoka.

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu

Mkuu wa shirika la UN kwa wakimbizi wa Palestina alisema Jumapili kuwa Gaza “inanyongwa” na kuwa karibuni upatikanaji wa maji, chakula na dawa utakwisha.

“Shambulizi la Wiki iliyopita dhidi ya Israeli lilikuwa la kinyama,” aliwaambia waandishi wa habari.

“Shambulizi hilo na mateka ni ukiukaji wa dhahiri wa sheria za kimataifa. Lakini hoja ya mauaji ya raia haihalalishi kuua raia zaidi.”

Jeshi la Israeli lilisema Jumatatu idadi ya waliotekwa nyara na kuchukuliwa Gaza baada ya shambulizi la October 7 lililofanywa na Hamas lilifikia watu 199, idadi iliyoongezeka kutoka ile ya awali iliyotolewa ya 155.

“Juhudi za kuwaokoa mateka ni kipaumbele cha juu kwa taifa,” msemaji wa jeshi Rear Adm. Daniel Hagari alisema.

“Jeshi hilo na Israeli wanafanya kazi usiku na mchana kuwarejesha mateka hao.”

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres amewataka Hamas kuwaachia mateka hao mara moja bila ya masharti yoyote.

Pia ameisihi Israeli kuruhusu bila pingamizi upitishaji wa mahitaji ya kibinadamu na wafanyakazi kufika Gaza.

Baadhi ya taarifa katika ripoti hii inatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.

Forum

XS
SM
MD
LG