Wanajeshi 63 wa Russia wauawa na makombora yaliyopigwa na Ukraine

Uharibifu uliyotokea kufuatia shambulizi la eneo la Makiivka, Ukraine.

Russia imesema Jumatatu kwamba  wanajeshi wake 63 wameuawa katika mkesha wa Mwaka Mpya katika  mashambulizi ya  makombora  ua Ukraine kwenye  eneo walipo mjini Makiivka eneo linalodhibitiwa na Russia ambalo ni sehemu ya mkoa wa Donetsk, Ukraine.

Tangazo la vifo hivyo ambalo si la kawaida kutolewa na Wizara ya Ulinzi ya Russia limekuja wakati Russia ikiendelea na mfululizo wa mashambulizi ya anga katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, licha ya Meya Vitali Klitschko kusema droni zote 40 zilizokuwa zinaulenga mji huo na maeneo ya jirani zilikuwa zimetunguliwa.

Wizara ya Ulinzi ya Russia ilisema Ukraine ililishambulia eneo la Makiivka kwa roketi nne kati ya sita kutoka katika mfumo wa makombora ya roketi yanayobebwa na magari yenye shabaha kali (HIMARS) ambapo Marekani imetoa mfumo huo kwa jeshi la Ukraine. Russia ilisema imetungua makombora mawili yaliyopigwa dhidi yao.

Jeshi la Ukraine halikuthibitisha moja kwa moja kuhusu shambulizi hilo lakini kimya kimya lilikiri kutokea na kudai kuwa lilikuwa baya zaidi kuliko Russia ilivyoripoti.

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Kimkakati ya Jeshi la Ukraine imesema Jumapili kuwa takriban wanajeshi 400 wa Russia waliuawa katika jengo la shule ya ufundi huko Makiivka na zaidi ya wanajeshi 300 walijeruhiwa. Taarifa iliyotolewa na Russia ilisema shambulizi hilo lilitokea “ katika eneo la Makiivka” na haikuitaja shule ya ufundi.

Daniil Bezsonov, afisa wa ngazi ya juu aliyewekwa na Russia katika maeneo yanayodhibitiwa na Moscow ya mkoa wa Donetsk, alisema jengo hilo lililokuwa ni makazi ya wanajeshi wa Russia lilikuwa “limeharibiwa vibaya sana.”

“Kulikuwa na waliopoteza maisha na waliojeruhiwa, idadi kamili bado haijulikani,” Bezsonov alisema kwenye ujumbe wake kwa njia ya Telegram “Jengo lenyee liliharibiwa vibaya sana.”

Baadhi ya taarifa hizi zinatokana na mashirika ya habari ya AP na Reuters.