Tanzania : Mbowe, Matiko wa Chadema warejeshwa rumande

Viongozi wa Chadema akiwemo Freeman Mbowe na Ester Matiko.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Chadema Tarime Mjini, Ester Matiko wataendelea kukaa rumande hadi rufaa ya kupinga dhamana iliyokatwa na upande wa mashtaka itakapoanza kusikilizwa katika Mahakama ya Rufaa Februari 18, 2019.

Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana zao Novemba 23, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya kukiuka masharti ya dhamana.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; mbunge wa Kibamba, John Mnyika; katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji;mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Wengine ni naibu makatibu wakuu Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara); mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018 jijini Dar es Salaam.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa serikali Wankyo Simon ulidai kuwa kesi hiyo imepangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba wanasubiri rufani iliyopo Mahakama ya Rufaa.

Hakimu Mhina alisema kwa sababu kesi hiyo imepangwa kutajwa mahakamani hapo, washtakiwa waliopo nje kwa dhamana wataendelea na dhamana na Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko wataendelea kukaa ndani hadi uamuzi wa rufani utakapotolewa.