Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Oktoba 04, 2024 Local time: 00:05

Zawawi, mtalaamu wa lugha ya Kiswahili, aaga dunia Zanzibar


Profesa Sharifa Zawawi akiwa Omar Zubeir mmoja wa ndugu zake nyumbani kwake Zanzibar.
Profesa Sharifa Zawawi akiwa Omar Zubeir mmoja wa ndugu zake nyumbani kwake Zanzibar.

Profesa aliyestaafu wa lugha za Kiswahili, Kiarabu na utamaduni na mila za Mashariki ya Kati, Sharifa Zawawi ameaga dunia huko Zanzibari.

Profesa atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa kueneza na kusomesha Kiswahili katika vyuo vikuu vya Marekani kabla ya kifo chake Jumanne huko Zanzibar.

Akiwa Profesa wa muda mrefu katika vyuo vikuu vya Columbia na New York, marehemu Zawawi alikuwa pia mshauri na mkaguzi wa mitihani ya vyuo mbali mbali vya Marekani.

Ameandika vitabu kadhaa vya kusomesha na kufahamisha lugha ya Kiswahili ambapo kimoja wapo mashuhuri ni "Kiswahili kwa Kitendo" kilichochapishwa kwa mara ya kwanza 1980 na kutumiwa kusomesha Kiswahili Marekani na Ulaya kwa wingi zaidi kuliko vitabu vingine vyote. Miongoni mwa vitabu vyake ni "Jifunze Kiswahili Chetu", "Converse in Kiswahili", "What’s in a Name?", "Unaitwaje?", na vitabu vingine

Zawawi mzaliwa wa Zanzibar mwenye asili ya Oman alifanya uchunguzi mrefu juu ya Kanga na kuandika kitabu juu ya historia yake na utamaduni wa watu wanaotumia nguo hiyo, aliyoeleza katika kitabu chake, Kanga, The Cloth that Speaks.

Walimu wenzake na wanafunzi wake wanamueleza kuwa mtu aliyekuwa na ujuzi na maarifa ya juu ya lugha hasa Kiswahili na msomi aliyefahamu utamaduni wa mswahili.

Abdul Nanji Profesa mwenzake mjini New York anamueleza Zawawi kuwa mtu mkarimu aliyewapenda na kuwaheshimu wanafunzi wake akiwa myenyekevu na mkaribu.

Anasema Profesa aliwasili Marekani baada ya uhuru wa Tanzania miaka ya 1960 na amekuwa akishiriki kwa karibu sana na jamii ya Waafrika Mashariki, akichangia kwa hali na mali mipango na juhdi zote za kuendeleza jamii yake.

Wanafunzi wake wanamkumbuka Bibi Zawawi kwa kuwahimiza kutamka lugha ya Kiswahili kama waswahili wenyewe. Mola amlaze pema peponi.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC

XS
SM
MD
LG