Polisi wa Malawi wameimbia VOA Jumapili kwamba wenzao wa Zambia walimkabidhi raia huyo wa China Lu Ke Jumamosi usiku katika wilaya ya Mchinji ambayo inapakana na Zambia.
“Yuko katika jela la polisi. Alikabidhiwa na marafiki zetu wa Zambia. Kufikia sasa amefunguliwa mashtaka ya usafirishaji haramu wa binadamu, lakini mashtaka mengine yanaweza kuongezwa”, amesema Harry Namwaza, naibu msemaji wa idara ya polisi ya Malawi.
Lu Ke alitoroka Malawi mwezi uliopita ambako polisi walikuwa wakimsaka baada ya uchunguzi wa shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) kubaini kwamba alikuwa akiwarekodi vijana wa vijijini katikati mwa Malawi na kuwafanya wazungumzie mambo ya kibaguzi yanayowahusu wenyewe katika lugha ya China ya Mandarin.
Katika video moja, watoto hao, baadhi yao wakiwa na umri wa miaka 9 wanasikika wakisema katika lugha ya Mandarin kwamba wao ni “mnyama mkubwa sana mweusi” na wana “kiwango cha chini cha uelevu.”
BBC iliripoti kwamba alikuwa anauza video hizo hadi dola 70 kila moja kwenye mitandao ya China. Watoto waliocheza katika video hizo walilipwa nusu ya dola moja kila mmoja.
Kufikia jana Jumapili, maafisa wa China walikuwa hawajatoa maelezo yoyote kuhusu kurejeshwa kwa Lu Ke.
Hata hivyo, msemaji wa polisi Namwaza amesema Lu Ke anatarajiwa kufika mahakamani hivi karibuni.