Maafisa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wanasema waasi wa Uganda wameuwa zaidi ya watu 21 katika mkoa wa Kivu Kaskazini. Shirika la habari la Ufaransa linaripoti kuwa wengi wa waliouawa usiku wa kuamkia Jumamosi walikuwa wanawake na watoto ambao walikatakatwa au kupigwa kwa virungu hadi kufa.
Mauaji hayo yalifanyika kilomita 45 kutoka kijiji cha Beni ambako watu 26 waliuawa mapema wiki hii. Maafisa wa DRC wanasema waasi wa Uganda wanaofanyia shughuli zao mashariki mwa nchi ndiyo waliohusika katika mauaji hayo.
Yaaminika waasi hao wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) wanafanyia operesheni zao kwenye mpaka wa DRC licha ya kuwepo kwa vikosi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa na vile vya serikali ya Congo.
Tume ya Umoja wa Mataifa nchini humo haijatoa taarifa kuhusiana na shambulizi la hivi karibuni.