Benki ya Dunia inasema imezuia fedha za Ivory Coast, ambako rais asiyetambulika aliye madarakani Laurent Gbagbo anaendelea kukumbatia madaraka licha ya kutokubaliwa na dunia nzima.
Rais wa Benki ya Dunia Robert Zoellick alitangaza usitishaji huo wa fedha za Ivory Coast Jumatano baada ya mazungumzo na Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy huko Paris.
Hatua hiyo inaongeza msukumo kwa bwana Gbagbo kukabidhi madaraka kwa mpinzani wake Alassane Ouattara, mshindi anayetambulika kimataifa katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi uliopita.
Mapema Jumatano, Ufaransa iliwasihi raia wake kuondoka Ivory Coast baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon kuonya kuwa nchi hiyo inakabiliwa na hatari ya kurudi kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Bwana Ban Jumanne alisema hali huwenda ikawa mbaya ndani ya siku kadhaa na aliyashutumu majeshi yanayomtii bwana Gbagbo kwa kujaribu kuzuia shughuli za Umoja wa Mataifa nchini Ivory Coast.
Benki ya Dunia yaweka vikwazo kwa Ivory Coast
