Matshidiso Moeti amekuwa mkuu wa afisi za WHO barani Afrika tangu Februari mwaka 2105 wakati ambapo mlipuko Ebola ulikuwa umetandaa huko Afrika magharibi. Kama mkuu wa idara ya WHO katika kanda hiyo, anasema alijuwa kuwa lazima afanye kila awezalo kusitisha kuenea kwa ugonjwa huo hatari.
Ameiambia VOA kwamba Liberia, Sierra Leone na Guinea wameboresha kwa kiasi kikubwa uwezo wao wa kujibu janga la Ebola. Anasema hii imedhihirishwa kwa njia zenye ujuzi walizotumia kusitisha kesi za hapa na pale za kuibuka tena kwa ugonjwa huo.
Bi Moeti anasema, wameweza pale walipopata kesi ambayo haikutarajiwa katika miezi ya michache iliyopita kushughulikia vilivyo na kutambua mapema, na kujaribu kuzuia kuenea kwa ugonja huo. Kwa hivyo kwangu mimi hilo ni mojawapo ya mambo bora yaloweza kupatikana kutokana na janga hilo huko Afrika Magharibi.
Lakini Bi Moeti ametahadharisha kuwa mabadiliko yalofanywa katika miundo mbinu, katika mfumo wa majibu ya haraka na mafunzo lazima yaendelezwe. Anasema hili linahitaji kuendelezwa kwa msaada wa jumuiya ya kimatiafa. Anasema ufadhili na utaalamu ulomiminika Afrika Magharibi wakati wa mlipuko wa Ebola lazima uwendelee.
Bi Moeti anasema, anamatumaini makubwa kuwa baadhi ya nia ya dhati zilizotolewa na wafadhili wakati ambapo mataifa hayo yalikuwa yakizungumzia kufufuka kutokana na janga hilo zitakamilishwa kwa sababu fedha hizo ni muhimu katika kuhakikisha wafanyakazi wa afya, miundo mbinu, maabara na vifaa vinavyohitajika vinaendelea kupatikana.
Baraza kuu la shirika la afya duniani WHO ambalo limemaliza mkutano wake wa mwaka hivi karibunii, limeidhinisha mageuzi katika mfumo wa dharura wa afya. Bi Moeti anapongeza makubaliano na nchi wanachama ya kutowa fedha zinazohitajika kutekeleza mfumo huu. Anasema WHO itakuwa katika nafasi bora kuepusha mizozo kabla haijawa mikubwa. Anasema hili litadhihirisha kuwa jambo la manufaa kwa nchi za kiafrika.