Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 16:49

Waziri wa Miundombinu Zanzibar ajiuzulu


Rais Mohammed Shein akipewa maelezo baada ya ajali ya MV Skagit July 19, 2012
Rais Mohammed Shein akipewa maelezo baada ya ajali ya MV Skagit July 19, 2012

Ni mara ya kwanza katika muda wa miaka mingi nchini Tanzania kwa waziri kujiuzulu kufuatia makosa yaliyofanywa ndani ya wizara yake

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano katika serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Hamad Masoud amejiuzulu wadhifa huo kwa sababu zinazohusiana na ajali ya meli ya abiria ya MV Skagit iliyouwa watu wapatao 88 wiki iliyopita.

Katika mahojiano na Sauti ya Amerika Waziri Masoud alisema amechukua uamuzi wa kuwajibika kisiasa kwa sababu ajali ya meli hiyo imetokana na hitilafu au utendaji mbaya katika wizara yake.

Alisema alimwandikia Rais wa Zanzibar Mohammed Shein Julai 20 kumweleza nia yake ya kujiuzulu na rais alimjibu Julai 23 kuwa anakubali kujiuzulu huko.

Bwana Masoud alisema ingawa yeye hakuwa mtendaji katika operesheni za meli hiyo au usafiri wa baharini anawajibika kama waziri katika wizara inayosimamia shughuli hizo.

Alipoulizwa kama ana habari endapo kuna watendaji wengine ambao watajiuzulu au kuwajibishwa Masoud alisema hayo yatatokana na ripoti atakayopelekewa waziri na tume iliyoundwa kuchunguza ajali hiyo.

Idadi ya watu wanaojulikana kufariki kutokana na ajali ya MV Skagit hadi sasa ni watu 88 lakini kuna wengine wasiozidi 100 ambao hawajulikani walipo mpaka sasa.

XS
SM
MD
LG