Mahakama ya kimatiafa ya uhalifu kwa Rwanda – ICTR iliyoko nchini Tanzania inayoungwa mkono na umoja wa mataifa imemhukumu Pauline Nyiramasuhuko kwa kuhusika kwake katika mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994. Ni mwanamke wa kwanza kuhukumiwa na mahakama hiyo.
Nyiramasuhuko amekutwa na hatia ya kuhusika na mauaji ya halaiki, njama za kutenda mauaji ya halaiki na ubakaji ikiwa ni uhalifu dhidi ya binadamu.
Nyiramasuhuko alikuwa waziri wa masuala ya wanawake na familia wakati watu laki 8 wa kabila la watusi na Wahutu wenye msimamo wa kadri walipouawa katika kipindi cha miezi mitatu. Alishitakiwa kwa kuamuru na kusaidia katika ukatili uliotokea katika mkoa wa kusini wa Butare wakati wakati wa mauaji hayo.
Mtoto wake wa kiume Arsene Shalom Ntahobalim pia alihukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama hiyo kwa makosa kama hayo. Maafisa wengine wanne walihukumiwa vifungo vya kati ya miaka 25 na maisha jela.