Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Februari 06, 2023 Local time: 05:27

Waziri wa fedha wa Marekani akamilisha ziara yake Zambia


Waziri wa fedha wa Marekani, Janet Yellen, katika ziara yake nchini Zambia.

Katika siku ya mwisho ya ziara yake nchini Zambia, Waziri wa fedha wa Marekani, Janet Yellen, alizngumzia changamoto ya hali ya hewa katika uzalishaji wa chakula na msukosuko wa kimataifa kutokana na vita vya Russia dhidi ya Ukraine. 

Katika siku yake ya pili akiwa Zambia, waziri wa fedha wa Marekani, Janet Yellen amesema njaa na uhaba wa chakula vinaleta madhara makubwa kwa jamii duniani kote.

Waziri Yellen, alisema ni kwa sababu hii Marekani inachukua hatua kali na za haraka ili kukabiliana na baa la njaa.

Yellen alizungumza Jumanne akiwa Chongwe, mashariki mwa mji mkuu wa Zambia, Lusaka, ambako alikutana na wakulima kadhaa wa kike kupitia mfuko wa hali ya hewa ya kijani, ambao Marekani inasaidia kupitia Umoja wa Mataifa.

Mradi huo wa Ustahimilivu wa Hali ya Hewa wa Maisha ya Kilimo katika Mikoa ya Kilimo na Ekolojia ya Zambia, unalenga kuwasaidia wakulima wadogo kudhibiti vyema athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika kupunguza njaa.

Anasema "idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula imeongezeka hadi milioni 345 katika nchi 80. Kwa Zambia, takriban watu milioni 2 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na karibu nusu ya watu hawawezi kukidhi kiwango cha lishe kwa kila siku.”

Waziri Yellen, pia aligusia vita vya Russia dhidi ya Ukraine kuwa vimesababisha usumbufu mkubwa wa usambazaji wa chakula kote duniani.

Alisema Marekani itafanya kazi kwa karibu na nchi za Kiafrika kama Zambia kuendeleza uwezo wake wa miundombinu na vifaa.

Alisisitiza kuwa bara la Afrika linahitaji uwezo thabiti sio tu kulima chakula, lakini kuhakikisha kuwa kinaweza kulimwa, kuhifadhiwa na kusafirishwa kwa ufanisi.

Anasema “hali hii ngumu imezidishwa na vita haramu vya Russia, dhidi ya Ukrainia, ambavyo vimesababisha bei ya mafuta na mbolea kupanda maradufu ulimwenguni."

Waziri Yellen katika ziara hiyo ya Chongwe, alikuwa pamoja na kaimu waziri wa kilimo wa Zambia, Gary Nkombo, ambaye alitoa shukrani kwa msaada wa Marekani kwa Zambia.

Nkombo alisema takriban familia 150 zimenufaika na mpango unaoongozwa na Umoja wa Mataifa katika eneo la Chongwe, unaoangazia kilimo cha uhifadhi.

Mwezi uliopita, zaidi ya viongozi 40 wa Afrika walikutana na wajumbe wa utawala wa Marekani mjini Washington, ambao waliahidi kuimarisha uwekezaji kati ya Afrika na Marekani.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG