Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 02:03

Waziri mkuu wa Somalia atoa wito wa utulivu baada ya ghasia


Mohamed Hussein Roble waziri mkuu wa Somalia
Mohamed Hussein Roble waziri mkuu wa Somalia

Waziri mkuu Roble anasema alisikitishwa na ghasia za usiku wa jumapili katika mji mkuu, Mogadishu, kati ya vyombo vya usalama vya serikali na vikosi vya upinzani. Aliongeza kuwa mazungumzo na kuelewana ndio njia pekee za kutatua mkwamo wao.

Mapigano yaliripotiwa nyumbani kwa kiongozi wa chama cha upinzani cha Wadajir Abdulrahman Abdishakur, na nyumbani kwa Rais wa zamani Hassan Sheikh Mohamud. Rais huyo wa zamani ni miongoni mwa wale wanaopinga kuongezwa kwa muda wa Farmajo.

Viongozi wa upinzani wa Somalia wamemlaumu Farmajo na vikosi vya usalama kwa mapigano hayo, lakini Waziri wa Usalama Hassan Hundubey anakanusha madai hayo na kulaumu upinzani.

Mzozo huo unahusiana na uchaguzi uliocheleweshwa. Uchaguzi wa bunge na urais wa Somalia umecheleweshwa kwa miezi kadhaa kwa sababu ya mizozo juu ya mchakato wa uchaguzi.

Mkwamo huo ulichukua sura mpya mwezi huu baada ya bunge kuu kupiga kura ya kuongeza muda wa mamlaka ya serikali ya Rais Farmajo kwa miaka miwili.

Wabunge wa upinzani, ambao tayari walikuwa wakipinga kukaa kwa Farmajo madarakani, walipinga vikali hatua hiyo wakati jumuiya ya kimataifa pia ilionya juu ya athari zake kwa uthabiti wa Somalia.

Mohamed Hassan Idris, mwanachama wa chama cha upinzani, anasema serikali haiko tayari kwa mazungumzo kutokana na hatua zake kuhusu ghasia katika mji mkuu.

Umoja wa Afrika wiki iliyopita uliwataka viongozi wa Somalia kuanza tena mazungumzo ya uchaguzi, wakikataa agizo la kuongezwa muda kwa Farmajo.

Mjumbe wake anatarajiwa kuzuru Somalia katika wiki zijazo. Afyare Elmi ni profesa mshirika wa masomo ya usalama katika chuo kikuu cha Qatar. Anasema mazungumzo ndiyo njia pekee ya kuepuka mapigano ya silaha yaliyoonekana huko Mogadishu siku ya Jumapili.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia ilitoa wito wa kusitisha ghasia kwa pande zote, huku ikitoa wito kwa pande hizo kuanza mazungumzo mara moja.

XS
SM
MD
LG