Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 19, 2024 Local time: 04:36

Waziri mkuu wa Israel asema tarehe ya kuushambulia mji wa Rafah imepangwa


Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, alisema Jumatatu kwamba tarehe ya mashambulizi ya ardhini, yakilenga mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah, imepangwa, lakini bila kutaja ni lini.

Hayo yalijiri huku White House ikisema wapatanishi wake mjini Cairo, walikuwa wamewasilisha kwa wanamgambo wa Hamas, pendekezo la mpango wa kusitisha mapigano, na kuachiliwa kwa mateka.

"Leo, nilipokea ripoti ya kina kuhusu mazungumzo ya Cairo," kiongozi huyo wa Israel alisema huko Jerusalem.

"Tunajitahidi sana ili kufikia malengo yetu, kwanza kabisa kuachiliwa kwa mateka wetu wote, na kupata ushindi kamili dhidi ya Hamas. Ushindi huu unajumuisha kuingia Rafah na kutokomeza vikosi vya kigaidi vilivyoko huko. Tarehe imepangwa," alisema Netanyahu.

Mara moja Marekani ilimkemea kiongozi huyo wa Israeli kufuatia kauli hiyo. Msemaji wa wizara ya ulinzi alisema "Tumeweka wazi msimamo wetu kabisa kwamba hatuungi mkono operesheni za Rafah."

"Tunataka kuona mpango wa kuaminika wa jinsi watakavyoendesha shughuli zozote huko" kutokana na wasiwasi "mkubwa" wa kibinadamu, kuhusu zaidi ya raia milioni moja wa Kipalestina walio huko, alisema naibu msemaji wa Pentagon Sabrina Singh.

Forum

XS
SM
MD
LG