Mjadala wa tuhuma za ubadhilifu wa fedha za serikali katika bunge la Tanzania uimechukua sura mpya baada ya mbunge wa kambi ya upinzani Zitto Kabwe kukusanya saini ya asilimia 20 ya wabunge ili kuwasilisha hoja ya kupiga kura ya kutokuwa na imani ya serikali.
Mbunge kabwe amesema katika kanuni za bunge ibara ya 123 inataka kuwepo na asilimia hiyo ili kutoa fursa sahihi ya kuwasilisha kwa spika wa bunge kusudio la hoja ya kutokuwa na imani na waziri mkuu.
Asilimia 20 ni sawa na wabunge 70 zoezi lililotarajiwa kufanyika kwa siku tatu .
Tayari wabunge 73 wameshatoa sahihi zao na hoja hiyo itawakilishwa kwa spika wa bunge la Tanzania bi Anne Makinda jumatatu ijayo ili aweze kuruhusu hoja hiyo ijadiliwe bungeni ambapo inahitajika zaidi ya nusu ya wabunge ili kuweza kupitisha hoja hiyo.
Amesema sababu kubwa ya kuamua kuchukua hatua hiyo ni kutokana na ubadhilifu na matumizi mabaya ya fedha za umma ambayo yameripotiwa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali yakihusisha mawaziri watano. Waziri mkuu wa Tanzania alitolewa mwito wa kuwafukusa kazi mawaziri hao hatua ambayo bado hajaitekeleza.