Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 18:28

Majaliwa achukua sampuli za mchanga kutoka mgodi wa Buzwagi


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amechukua sampuli za mchanga katika makontena mbalimbali ambao utapelekwa kwa wataalamu wa madini kupimwa ili kubaini kiasi cha dhahabu kilichomo katika mchanga huo.

Wakati anafanya ziara hiyo katika mgodi wa dhahabu wa Buzwagi uliopo wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga amesema wanataka kujua mchanga unaosafirishwa na mwekezaji huyo unakiasi gani cha dhahabu.

Waziri Mkuu pia amesema “Serikali inataka kufahamu kama kodi inayolipwa ni sahihi.”

Hata hivyo tayari Rais Dkt. John Magufuli alishatoa tangazo la kuzuia usafirishaji wa mchanga kwenda nje ya nchi, na kutoa amri kwamba makontena yaliyokuwa yako bandarini na mchanga wenye madini ndani kuwa upimwe.

Waziri Mkuu alitembelea mgodi huo jana jioni (Jumatatu, Machi 27, 2017) na kuchukua sampuli za mchanga kwa lengo la kuondoa mashaka juu ya kinachosafirishwa. Sampuli hizo amezichukuwa kwenye makontena yaliyofungwa kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Tumeamua kuchukua sampuli za mchanga ambao mwekezaji anasema wanaupeleka nje ya nchi kwa ajili ya kwenda kutenganisha madini ya dhahabu na shaba. Hata hivyo nimemuhoji kwa nini mitambo hiyo isiletwe nchini ili kila kitu kifanyike hapahapa.”

Waziri Mkuu amesema sera ya uwekezaji inasema mtambo huo unatakiwa uwepo nchini ili kila hatua ya utenganishaji ifanyike hapa hapa, hivyo tunataka kujiridhisha na mwenendo wa mwekezaji na mapato tunayoyapata kama yanastahili.

Aliongeza kwamba “Hili lipo miongoni mwa masharti ya uwekezaji kwenye sekta ya madini nchini kwamba mitambo hiyo ije kujengwa hapa nchini na itaongeza fursa ya ajira na kukuza sekta nyingine ikiwemo ya kilimo.”

Wakati huohuo Waziri Mkuu amewataka Watanzania kuwa nasubira wakati Serikali ikiendelea na zoezi la kuchunguza athari zitokanazo na kusafirisha mchanga wa madini nje ya nchi. Pia amewatoa wasiwasi wafanyakazi katika migodi na wamiliki kutowapunguza na badala yake waache waendelee na majukumu yao.

Kwa upande wake Meneja Uendelezaji wa mgodi huo George Mkanza amesema mgodi huo ulionzishwa mwaka 2009 umeajiri watumishi 720 pamoja na vibarua 500.

Amesema kwa siku wanachenjua makontena matatu hadi sita ambapo katika kila kontena moja wanapata kilo tatu za madini ya dhahabu na tani nne za madini ya shaba.

Mkanza amesema wanazalisha asilimia 50 ya madini ya dhahabu na asilimia 50 ya dhahabu iko kwenye mchanga na inakuwa imechanganyika na madini ya shaba ambayo ndiyo unaosafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutenganishwa.

“Hapa Buzwagi tuna makontena 179, makontena mengine 152 yako Dar es Salaam kwenye bandari kavu ya Nazam na 21 yako bandarini. Kila siku tunapoendelea kuzalisha tunakuwa na makontena manne hadi sita. Ndugu zetu wa Bulyanhulu nao wanamakontena 108 yako mgodini na 104 yako Nazam Cargo Dar es Salaam,” amesema.

XS
SM
MD
LG