Mlinzi mmoja alimpiga risasi na kumuua waziri wa serikali nchini Uganda mapema Jumanne katika mzozo unaoonekana kuwa wa kibinafsi kulingana na jeshi na vyombo vya habari nchini humo.
Mshambuliaji huyo ambaye hajatajwa hadharani kisha akajipiga risasi kwa mujibu wa shirika la utangazaji la UBC na vyanzo vingine vya habari.
Mwathiriwa Charles Engola, alihudumu katika serikali ya Rais Yoweri Museveni kama naibu waziri anayehusika na kazi. Alikuwa kanali mstaafu wa jeshi.
Msemaji wa jeshi Brig. Felix Kulayigye alisema katika taarifa fupi kwamba ni tukio kusikitisha lililosababisha mauaji ya Engola. Tutafahamisha umma maelezo zaidi tunapochunguza kwa pamoja suala hili Kulayigye alisema kwenye mtandao wa Twitter.
Shambulizi hilo lilifanyika ndani ya nyumba ya Engola katika kitongoji cha mji mkuu wa Uganda, Kampala. Wapelelezi wa polisi wanaendelea na uchunguzi.
Sababu ya shanbulizi hilo haikujulikana mara moja, lakini vyombo vya habari nchini humo vilisema kumekuwa na mzozo juu ya mishahara ya mlinzi huyo.