Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Oktoba 08, 2024 Local time: 08:35

Wawili watuhumiwa kwa kutaka kumuua Theresa May


Eneo lenye ulinzi la mageti ya kuingilia ofisi za Downing Street, London.
Eneo lenye ulinzi la mageti ya kuingilia ofisi za Downing Street, London.

Wanaume wawili wamefikishwa Mahakamani Jumatano mjini London kwa tuhuma za ugaidi kutokana na madai kuwa walipanga kumuua Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May, kwa mujibu wa maelezo ya maafisa wa serikali ya Uingereza.

Maafisa hao wamesema kuwa watu hao walishirikiana kutaka kufanya shambulizi la kutumia kisu katika eneo la Downing Street, ambapo ni makazi rasmi ya Waziri Mkuu.

Habari ya kuzuiliwa mpango wa kufanya mauaji hayo ulijulikana muda mfupi baada ya mkuu wa usalama wa ndani M15 nchini Uingereza, Andrew Parker, kutoa taarifa kwa baraza la mawaziri juu ya tishio la shambulizi la kigaidi.

Kadhalika aliwafahamisha mawaziri kuwa idara yake iliweza kuzuia mashambulizi tisa mwaka 2017. Hata hivyo taarifa hizi zilichukuwa masaa kadhaa kuvifikia vyombo vya habari.

Wahusika wa jaribio hilo walikamatwa wiki iliyopita katika msako uliofanywa na maafisa wanaopambana na ugaidi London na Birmingham, maafisa wa polisi wamesema. Mmoja wa watu hao waliokamatwa, aliyetajwa jina lake ni Naa’imur Zakariyah Rahman, miaka 20, anatuhumiwa kwa kuandaa vitendo vya ugaidi.

Alipokamatwa Uingereza Novemba 28, inadaiwa kuwa alikuwa amebeba mabomu yakutengeneza mwenyewe, yaliyokuwa hayana nguvu. Mshukiwa mwenziwe katika uhalifu huo ametajwa ni Mohammed Aqib Imran, miaka 21. Yeye alikamatwa dakika 90 baadae katika msako ulofanyika katika nyumba moja eneo la Birmingham huko mji wa English Midlands.

Imran anatuhumiwa pia kwa kujaribu siku za nyuma kupata pasi ya kusafiria ya kughushi katika juhudi zake za kwenda Libya kuungana na kikundi cha Islamic State chenye mafungamano na makundi yaliyoko nchi Afrika Kaskazini.

Kwa mujibu wa maafisa wa serikali watu hao wawili walikuwa wanapanga kufanya mashambulizi katika milango ya ulinzi inayolinda eneo la kuingilia ofisi za Downing Street. Rahman inadaiwa kuwa alipanga kuvamia katika eneo Number 10 lenye ofisi na makazi ya Waziri Mkuu, akiwa amevaa mabomu na kutumia pilipili kuwapulizia walinzi na kisu, akiwa na azma ya kumuua Theresa May.

XS
SM
MD
LG