Raia wa Uingereza Khuram Shazad Butt, mwenye miaka 27, alikuwa anajulikana na vyombo vya dola lakini alikuwa haonekani kama ni tishio kubwa kwa umma.
“Hapakuwa na taarifa zozote za kiusalama zilizopendekeza kuwa tukio la shambulio kama hili lilikuwa limepangwa na uchunguzi wa vitendo vya ugaidi ulikuwa umepewa kipaumbele kama kawaida nchini, Polisi imesema katika tamko lake.
Mshambuliaji wa pili ametambuliwa kuwa ni Rachid Reouane, mwenye umri wa miaka 30. Wote wawili walikuwa wanaishi katika eneo la London Mashariki, polisi wamesema.
Polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa mshambuliaji wa tatu kutambua wasifu wake.
Polisi London waliendelea kufanya msako zaidi Jumatatu na kuwatia nguvuni “idadi kadhaa” ya watu wakati uchunguzi katika maeneo kadhaa ya Newham na Barking yakiendelea.
Polisi wamesema kuwa shambulizi la Jumamosi lilifanywa na watu watatu waliokuwa ndani ya gari ambalo kwanza liliwagonga watembea kwa miguu katika daraja la London, kisha wakashuka na kuwachoma visu watu wengi katika soko lililokuwa karibu na eneo hilo kabla polisi kuwapiga risasi na kuwaua.
“Tunajaribu kujua iwapo kuna mtu yoyote alikuwa akiwasaidia na kujua historia ya shambulizi hili kwa kadiri ya uwezo wetu,” Mkuu wa kituo cha polisi cha Metropolitan Cressida Dick ameiambia Sky News.
Kikundi cha Islamic State kimedai kuhusika na shambulizi hili kupitia shirika lake la habari Amaq.