Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 09:46

Kenya: Wauguzi wakaidi amri ya rais kurudi kazini


Mgomo wa wauguzi waendelea Kenya
Mgomo wa wauguzi waendelea Kenya

Hata baada ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kuamuru wauguzi wote nchini kurejea kazini na kurejelea majukumu yao  Ijumaa la sivyo serikali za majimbo zianze mkakati wa kuwaondoa kazini, usitishwaji wa huduma za afya nchini humo kutokana na mgomo huo ulioanza Februari 4 mwaka huu bado unaendelea.

Mgomo huo unaendelea kusambaratisha utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa katika hospitali za umma nchini Kenya.

Japo baadhi ya majimbo yameafikia muafaka na wauguzi kutoka majimbo hayo, maeneo mengine yangali yanakabiliwa na changamoto za utoaji huduma hizo.

Akizungumza na vyombo vya habari Ijumaa jijini Nairobi, Waziri wa Leba Ukur Yattani alieleza kuwa serikali itafika mahakamani Jumatatu kutaka mahakama iwaadhibu wauguzi hao kwa kutofuata wito wa kurejelea majukumu yao.

Sikiliza

please wait

No media source currently available

0:00 0:03:16 0:00

Jopokazi la kuondoa utata huo lililobuniwa na serikali limeonekana kutoafikia chochote kufuatia ususiaji wa wawakilishi wa wauguzi katika mazungumzo hayo huku wakiyataja kuwa yasiyokuwa na umuhimu wowote.

Muungano wa wauguzi nchini Kenya ungali unasisitiza kuwa wauguzi watarejelea majukumu yao tu wakati wizara ya afya na serikali za majimbo zitawalipa wauguzi malimbikizi yao.

Hata hivyo, Baraza la Magavana Alhamisi lilisisitiza kuwa ufuatiliaji wa amri ya Rais Kenyatta utafanyika Ijumaa kubaini wale wanaofika kazini.

Muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini Kenya, COTU, sasa unamtaka Waziri Ukur Yattani kujiuzulu kwa "kumpotosha rais Kenyatta."

Francis Atwoli, Katibu Mkuu wa Muungano huo anasisitiza kuwa wafanyakazi wana haki ya kugoma.

Utata huu unafungamana na madai ya wauguzi kueleza kuwa serikali za majimbo zimejikokota kutoa mwongozo wa kutekeleza makubaliano ya kurejea kazini yalioafikiwa mnamo Novemba 2, 2017 kama njia ya kupiga marufuku mgomo wa wauguzi hao uliodumu kwa zaidi ya miezi mitano mwaka wa 2017.

-Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Mwandishi wa Sauti ya Amerika, Nairobi, Kenya.

XS
SM
MD
LG