Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 26, 2024 Local time: 10:53

Watuhumiwa 13 wa Dawa za Kulevya Chini ya Uangalizi wa Polisi na Mahakama


Watuhumiwa wa kesi ya dawa za kulevya wakiingizwa mahakamani
Watuhumiwa wa kesi ya dawa za kulevya wakiingizwa mahakamani

Watuhumiwa 13 wa matumizi ya dawa za kulevya wakiwemo wasanii maarufu watakuwa chini ya uangalizi wa polisi na mahakama huku shauri linalomhusu msanii Wema Sepetu hatma yake ikiwa haijulikani.

Hata hivyo mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa watuhumiwa hao walifikishwa Mahakama ya Kisutu mapema Jumanne. Bado msanii Wema anashikiliwa katika kituo kikuu cha polisi jijini Dar es salaam.

Waliopandishwa Kizimbani

Baadhi ya watuhumiwa waliopandishwa kizimbani leo ni pamoja na Khaleed Mohamed (TID) , Hamid Salum Chambuso, Rachel, mrembo Tunda Kimaro, na Joan.

Watu wengine maarufu kadhaa nao inasemekana wanaendelea kuhojiwa juu ya tuhuma hizo za kujihusisha na dawa za kulevya.

Kupitia hati ya kiapo cha Jamhuri ya Tanzania, mahakama imetoa masharti ya watuhumiwa hao kuwa chini ya uangalizi wa jeshi la polisi na mahakama kati ya mwaka moja hadi mitatu kwa ajili ya kuangalia mwenendo wao.

Watuhumiwa Wala Kiapo

Upande wa jamhuri chini ya kiapo cha mkuu wa kitengo cha polisi cha kupambana na dawa za kulevya ASP Denis Mnyumba umeiomba mahakama kutoa kiapo kwa watuhumiwa ikiwemo uangalizi wa kipindi kisichozidi miaka 3 huku wahusika wakitakiwa kuripoti polisi mara mbili kwa mwezi,ili kufuatilia mwenendo wa tabia zao.

Hata hivyo watuhumiwa hao wametakiwa kuwekewa dhamana kwa viwango tofauti kati ya milioni 10 na milioni 20 na mpaka VOA inaondoka mahakamani hapo haikujulikana waliotimiza masharti ya dhamana.

Kilio cha Waathirika wa Madawa
Katika mahojiano na VOA baadhi ya watumiaji wa dawa za kulevya maarufu kama mateja katika eneo maarufu la Karume wameiomba serikali kuwarahisishia kupata tiba ya kupambana na athari za kuacha dawa za kulevya kuliko kuendelea kuwakamata na kuwaweka ndani.

Tangu wiki iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda alianzisha operesheni maalum ya kupambana na wanaojihusisha na dawa za kulevya ambapo mpaka jana watu zaidi ya 100 walikuwa tayari wamehojiwa.

XS
SM
MD
LG