Mapigano ya bunduki kati ya wanamgambo wa al-Shabab na makundi yanayoiunga mkono serikali yamesababisha vifo vya takriban watu 20 huko Somalia.
Afisa mmoja wa jeshi anasema mapigano hayo yalianza Alhamisi katika eneo la Bula Hawo, kwenye eneo la mpaka wa Ethiopia na Kenya . Mashahidi wanasema mapigano yaliendelea mpaka mapema Ijumaa asubuhi.
Majeshi ya serikali na vikosi vya Umoja wa Afrika vililichukua udhibiti wa ngome hiyo ya muda mrefu ya waasi mapema wiki hii. Wanamgambo hao walikuwa wanajaribu kuchukua tena ngome yao lakini makamanda wa serikali walisema Ijumaa kuwa waliwazuia na kuwafurusha.
Somalia iemshuhudia karibu miongo miwili ya ghasia na ukosefu wa utawala wa sheria tangu kupinduliwa kwa serikali ya mwisho ya Siad Barre.
Serikali iliyopo madarakani hivi sasa inakabiliwa na mivutano ya ndani na imefanikiwa kubaki madarakani kutokana na uungaji mkono mkubwa wa walinda amani wa Umoja wa Afrika.