Takriban watu wanne walipata majeraha ya risasi wakati polisi walipokabiliana na waandamanaji katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma, kaskazini mwa Kenya.
Maelfu ya wakimbizi katika kambi hiyo ambayo inawahifadhi watu wanaokimbia vita pamoja na ukame katika nchi jirani za Sudan Kusini, Ethiopia, Burundi na Congo, waliandamana Jumatatu kupinga mgao wa chakula kutokana na vikwazo vya ufadhili.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani-WFP ambalo linasimamia usambazaji wa chakula katika kambi za wakimbizi lilisema mwezi Desemba mwaka jana kuwa mgao wa chakula katika kambi za wakimbizi ulikuwa asilimia 45 ya kiwango cha chini cha chakula kutokana na upungufu wa rasilimali.
WFP imetoa tahadhari kwa miaka mingi kwamba inakabiliwa na upungufu wa michango kutoka kwa serikali ambazo inazitegemea kwa fedha na Jumatatu ilitangaza kuwa inafunga ofisi yake nchini Afrika Kusini kutokana na kupunguzwa kwa misaada ya kigeni ya Rais wa Marekani Donald Trump.
Forum