Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 17, 2024 Local time: 19:37

Watu 40 wauawa katika shambulio nchini Mali


Ramani ya Mali
Ramani ya Mali

Watu wasiojulikana waliwaua watu 40 katika shambulio kwenye kijiji kimoja katikati mwa Mali, maafisa wa eneo hilo walisema Jumanne.

Shambulio hilo lilifanyika Jumatatu katika kijiji cha Djiguibombo katika jimbo la Mopti, moja ya maeneo kadhaa ya kaskazini na katikati mwa Mali ambako makundi ya wanajihadi yenye uhusiano na al Qaeda na Islamic State yamekuwa yakiendesha uasi kwa zaidi ya mwongo mmoja.

“Lilikuwa shambulio baya, watu wenye silaha walikizingira kijiji na kuwapiga risasi watu,” alisema Meya wa mji wa Bankass Moulaye Guindo.

Hakuweza kuliambia shirika la habari la Reuters idadi ya vifo, lakini maafisa wawili wa eneo hilo waliozungumza kwa masharti ya kutotajwa majina, walisema watu 40 waliuawa.

“Yalikuwa mauaji ya kikatili, walikizingira kijiji ambako kulikuwa kunafanyika harusi. Kulikuwa taharuki, baadhi ya watu walifaulu kukimbia, lakini wengi waliuawa, wengi wao walikuwa wanaume,” alisema mmoja wa maafisa hao.

Hawakuweza kuwatambua washambuliaji na hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo.

Reuters haikuweza kumpata msemaji wa jeshi la Mali kwa maelezo zaidi.

Machafuko yameongezeka katika eneo la Sahel ya kati Afrika Magharibi tangu uasi wa wanajihadi kuweka mizizi nchini Mali na kuenea katika nchi jirani za Burkina Faso na Niger, na kuua maelfu ya watu na kuwahamisha kwenye makazi yao mamilioni ya wengine.

Forum

XS
SM
MD
LG