Watu wasiojulikana walishambulia na kulipiga risasi lori lililokuwa limebeba wafanyakazi wa Shirika la Maendeleo la Cameroon (CDC) - kampuni kubwa zaidi ya viwanda vya kilimo inayomilikiwa na serikali ambayo wafanyakazi wake walilengwa hapo awali na watu wanaotaka kujitenga wenye silaha wanaozungumza lugha ya Kiingereza wanaopigania taifa huru.
Shambulizi la kushtukiza lilifanyika mwendo wa saa 11na nusu jioni kwa saa za huko karibu na mji wa Tiko baada ya vibarua kumaliza kazi yao, alisema Gabriel Mbene Vefonge, rais wa Chama cha Wafanyakazi wa Kilimo na Washirika wa Cameroon (CAAWOTU).
"Kwanza walimpiga risasi dereva ili kulizuia gari. Waliwaua wafanyakazi wengine watatu waliokuwa wamekaa mbele kabla ya kufyatua risasi kiholela," Vefonge aliiambia Reuters kwa njia ya simu, na kuthibitisha kuwa watano waliuawa kwa jumla.
Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo. CDC, polisi, na mwakilishi wa wanaotaka kujitenga hawakujibu kutoa maoni zaidi.
Walionusurika katika shambulio hilo walikuwa wakitibiwa majeraha ya risasi katika Hospitali ya CDC Cottage Tiko, muuguzi wa eneo hilo alisema, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina na kukataa kutoa maelezo zaidi.
Mzozo wa kujitenga, ambao ulichochewa na miongo kadhaa ya kutengwa kwa jamii ya wanaozungumza lugha ya Kiingereza nchini Cameroon na serikali inayotawaliwa na wanaozungumza kifaransa uligeuka wa umwagaji damu mwaka 2017 baada ya maandamano ya kawaida kukandamizwa vikali.
Tangu wakati huo, maelfu ya watu wameuawa katika taifa hilo na waasi na wanajeshi wa serikali wamechukua zamu kufanya ukatili mbaya.
Mwezi uliopita, serikali ilisema haijatoa mamlaka kwa nchi yoyote kuwezesha mazungumzo na wanaotaka kujitenga ili kusaidia kumaliza mzozo huo, licha ya Canada kusema kuwa imepokea ombi la kufanyia kazi mchakato wa amani.
Facebook Forum