Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 13:34

Wasifu wa Mgombea wa urais John Katumba mwenye umri wa miaka 24


John Katumba mgombea kiti cha urais kijana nchini Uganda
John Katumba mgombea kiti cha urais kijana nchini Uganda

Mgombea kijana kuliko wote ni John Katumba, aliyezaliwa mwaka ambao rais Yoweri Museveni alichaguliwa kuwa rais kikatiba ambao ni 1996.

Anakuwa mgombea kiti cha rais mwenye umri mdogo si Uganda pekee yake bali Afrika nzima akiwa na lengo anasema la kumondoa madarakani Museveni ili kuleta mabadiliko ya kisaikolojia, kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Ni machache yanayo fahamika kuhusiana na maisha yake na hata ilikuwa vigumu kufahamu juu ya maisha yake alipozungumza na Sauti ya Amerika ili kutayarisha wasifu wake.

Kwenye mitandao ya kijamii nchini Uganda, mjadala umekuwa ukiendelea sana kumhusu Katumba, mwenye umri wa miaka 24.

Hajawahi kufanya kazi ya kuajiriwa kulingana na maelezo yake kwani amemaliza masomo ya chuo kikuu hivi karibuni lakini alifanikiwa kuzuru kote Uganda na kupata saini za wafuasi wake na kulipa shilingi milioni 20 zinazohitajika ili kuidhinishwa kama mgombea.

Kuhusu nani anaegharimia kampeni yake Katumba anasema, “Nilijiwekea akiba nyumbani na nikiona kwamba pesa zimetosha, nazipeleka benki.”

Katumba anadai kwamba alianza kujilipia karo akiwa katika shule ya upili hadi chuo kikuu kwa kufanya kazi ndogo ndogo ikiwemo kuosha magari.

“Nilichoma mkaa, nikatengeneza matofali ya kujenga na kuosha magari ili kupata pesa za kutosha kufanikisha ndoto yangu ya kugombea urais Uganda,” amesema Katumba bila kusema kiwango cha pesa ambacho aliweka kama akiba katika mkoba wake wa mbao nyumbani.

Mjadala kuhusu milioni 20 kwa Tume ya Uchaguzi

Katumba alipotangaza nia ya kugombea urais, mitandao ya kijamii ilijaa mjadala na kejeli, wengi wakisema kwamba ilikuwa ni utani. Lakini kadri siku zilivyosonga, ndivyo Katumba alionekana kwamba anamaanisha alichokisema.

Alipoidhinishwa na tume ya uchaguzi, mjadala ulienea kuhusu mahali amepata kiasi cha shilingi milioni 20 kulipa tume ya uchaguzi kwa uteuzi wake.

Mjadala pia ulienea namna alivyofanikiwa kuzuru wilaya 98 za Uganda kukusanya Saini 100 kufanikisha ndoto yake ya kugombea urais, ikitiliwa maanani kwamba kiasi cha shilingi milioni 20 ni ndoto kubwa kwa idadi kubwa ya watu nchini Uganda kupata.

Lakini anasisitiza kwamba alitumia akiba aliyokuya nayo na msaada kutoka kwa marafiki wake waliyemchangia wakati alipokuwa anakusanya saini.

“Baadhi ya watu walikuwa wakinitumia pesa kama shilingi 1000 ili kunisaidia kufanikisha shughuli hii. Nina watu wengi ambao walinipa kiasi kikubwa cha pesa lakini hawataki kutajwa. Walichangia kwa sababu wana Imani kwamba nitashinda kura za urais,” ameeleza Katumba.

Maisha ya Katumba

Maisha ya mgombea urais John Katumba yamezungukwa na usiri mkubwa san ana hayupo tayari kuyazungumzia katika mahojiano. Hata mahali anapoishi pia ni siri.

“Nina mahali ambapo naishi japo similiki wala sikodishi nyumba. Mimi ni kijana. Kama unanihitaji, nipigie simu na nitakwambia mahali tunaweza kukutana. Hiyo ni sawa?”

Namba yake ya kulipa ushuru ilisajiliwa siku moja kabla ya kuasilisha maombi ya kugombea urais na hivyo kupata rekodi kumhusu pia ni vigumu.

Ni mgeni kwenye mitandao ya kijamii na hivyo ni vigumu kufuatilia historia yake.

“Mimi ni mgeni kwa mambo mengi kwa sababu sina imani nayo. Kwa mfano, najiwekea akiba nyumbani kwangu kwa sababu mkebe wangu wa kuweka pesa hautaniomba riba jinsi ilivyo katika benki. Mimi ni mgeni kwa mitandao ya kijamii kwa sababu sisna hamu na kampuni zinazomilikuwa na mataifa ya magharibi. Ninapanga kufungua mitandao yangu ya kijamii. Kampuni yangu.” Amesema Katumba.

John Katumba mgombea kiti cha rais kijana nchini Uganda
John Katumba mgombea kiti cha rais kijana nchini Uganda

Je, Katumba ametumwa na wanasaisa maarufu kugawanya kura za vijana?

Baadhi ya raia nchini Uganda, wamekuwa wakidai kwamba John Katumba anatumiwa na baadhi ya wanasiasa maarufu kugawanya kura za vijana katika uchaguzi mkuu wa Novemba 3.

Mbunge wa manispaa ya Mukono Betty Nambooze, ameandika kwenye ukurasa wa Facebook kwamba “wale wanaokutaka wewe Katumba ugombee urais, wanadhani kwamba wanaweza kukutumia kugawanya kura za vijana na kutoka kabila la Baganda.”

Lakini Katumba anasema mjadala huo unaumiza sana fikra zake na kusisitiza kwamba hakuna mtu anayemtumia bali ana ufuasi mkubwa kote Uganda na anagombea urais ili kuleta mabadiliko mema Uganda.

“wagombea wengi wanafanya tu siasa badala ya kuleta uongozi. Upinzani umejaa watu wanaojitafutia makuu, na hawana mpango wowote kufanyia watu kazi,” amedai Katumba.

Kubuni ajira kwa vijana

Katika kampeni zake, Katumba anaahidi kubuni nafasi za kazi hasa kwa vijana.

“Mpango wangu ni kuifanya Uganda kuwa nchi iliyostawi kiviwanda ili kubuni nafasi kadhaa za ajira kwa watu wetu,” amesema Katumba bila kutoa maelezo zaidi namna atakavyofanikisha malengo yake.

John Katumba ni nani?

Japo anasema ana umri wa miaka 24, hataki kuzungumzia mwaka alipozaliwa na hataki kuulizwa maswali mengi kumhusu yeye.

Anasema anatoka familia ya mtu anaitwa Kkonde, jijini Kampala, lakini hataki kutoa maelezo zaidi kuhusu Kkonde.

“Napenda tu niseme kwamba natoka kwa familia ya Kkonde na sitaki kuzungumzia mengi. Naomba tuachie hapo.”

Katumba hana familia na anasema amemaliza masomo katika chuo cha biashara cha Makerere hivi karibuni. Alisomea usimamizi wa kusafirisha mizigo na kumaliza mwezi Januari mwaka 2020.

Amesoma katika shule ya msingi ya Zion wilayani Buikwe kabla ya kusoma katika shule ya upili ya Central view kwa masomo ya kidato cha nne na sita.

“wazazi wangu walikufa. Na sijui mengi kuwahusu. Ninachojua ni kwamba mlezi wangu aliniambia kwamba wazazi wangu walikuwa nikiwa na umri wa miaka 2.”

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG