Alisomea wilayani Soroti katika shule ya msingi na upili kabla ya kujiunga na chuo kikuu cha Makerere.
Alihitimu kutoka Chuo kikuu cha Makerere akiwa na shahada ya uzamili katika sayansi na uhandisi.
Ni mwalimu, mhandisi katika maswala ya ujenzi, mfugaji na mwanasiasa.
Alikuwa mbunge kwa muda wa miaka 15 akiwakilisha eneo bunge la Kumi. Wakati akiwa bungeni, alikuwa mwanachama wa kamati ya kazi na uchukuzi.
Kabla ya kuwa mbunge, alifanya kazi na kampuni mbalimbali za ujenzi na mashirika ya maendeleo katika jamii.
Aliingia katika siasa mwaka 1994 na kugombea nafasi ya ubunge bila mafanikio.
Kuongoza kampeni ya Ssemwogerere na Besigye
Mwaka 1996 alisimamia kampeni ya aliyekuwa mgombea wa urais Paul Kawanga Ssemwogerere katika majimbo ya Teso na Karamoja.
Amutriat alijiunga na aliyekuwa mgombea wa urais Dr. Kiiza Besigye mwaka 1999 na kuanza kampeni za kile waliita “kuleta mabadiliko ya uongozi nchini Uganda.”
Ni miongoni mwa waanzilishi wa chama kikuu cha upinzani cha Forum for democratic change – FDC.
Amekuwa mbunge kwa mda wa miaka 15 kuanzia mwaka 2001 hadi 2016.
Akiwa mbunge, alikuwa mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu sayansi na teknolojia pamoja na kamati ya kusimamia matumizi ya pesa katika taasisi za serikali.
Ni miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa utawala war ais Yoweri Museveni.
Alikuwa mratibu mkuu wa shughuli za kampeni ya Dr. Kiiza Besigye katika uchaguzi wa mwaka 2016.
Patrick Amuriat, aliteuliwa kuwa mgombea wa urais kupitia chama cha Forum for democratic change, baada ya Dr. Kiiza Besigye kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa msingi kwamba haina maana yoyote kushiriki uchaguzi ambao rais Yoweri Museveni ataiba na kutangazwa mshindi kisha baadaye mahakama iidhinishe ushinde wake.
Ujumbe wake katika kampeni unaangazia kuimarisha demokrasia, utawala bora, sekta za kilimo, kuimarisha ukuaji wa uchumi na kubuni nafasi za ajira hasa kwa vijana.
Imeyatarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC