Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 06, 2022 Local time: 03:26

Wasifu wa mgombea urais Gregory Mugisha Muntuyera


Mgombea urais Mugisha Muntu akiwa katika kampeni.

Meja Jenerali Gregory Mugisha Muntuyera anaejulikana kama Mugisha Muntu, alizaliwa mwezi Oktoba 1958 wilayani Ntungamo, magharibi mwa Uganda.

Baba yake alikuwa na ushirikiano mzuri sana na aliyekuwa rais wa Uganda hayati Milton Obote.

Alisoma katika shule za msingi na upili za wilayani Mbarara. Alisomea katika shule ya upili ya Makerere College kabla ya kusomea sayansi ya siasa katika chuo kikuu cha Makerere.

Alikuwa naibu wa rais wa muungano wa wanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere.

Ni kiongozi wa chama cha Alliance for National Transformation ANT ambacho alianzisha mwezi March mwaka 2019.

Kabla ya kuunda ANT, alikuwa kiongozi wa chama cha Forum for democratic change – FDC kati yam waka 2012 na 2017.

Wafuasi wa Mugisha Muntu wakimpokea wakati wa kampeni.
Wafuasi wa Mugisha Muntu wakimpokea wakati wa kampeni.

Aliondoka chama cha FDC mwezi Sepemba 2018 kutokana na kile alitaja kama tofauti ya msimamo namna ya kuendesha chama hicho, baada ya kushindwa na Patrick Oboi Amuriat katika uchaguzi wa chama.

Septemba 27 mwaka 2018, alitangaza kwamba alikuwa ameungana na wanasiasa wengine, wengi kutoka chama cha FDC, kuunda chama chao, ambacho baadaye kilizinduliwa kama ANT.

Kamanda wa jeshi la Uganda

Mugisha Muntu alikuwa kamanda wa jeshi la Uganda UPDF kati ya mwaka 1989 na 1998. Alikuwa kamanda wa jeshi hilo akiwa na umri wa miaka 29.

Aliwania uongozi wa chama cha Forum for democratic change FDC, mwaka 2008 na kushindwa na Dr. Kiiza Besigye.

Aligombea tena mara ya pili mwaka 2012 na kushinda.

Kujiunga na waasi

Muntu alijiunga na waasi wa National resistance army – NRA, wakiongozwa na Yoweri Museveni, mara tu alipomaliza mtihani wake katika chuo kikuu cha Makerere.

Rais Yoweri Museveni
Rais Yoweri Museveni

Hatua yake ilishangaza familia yake Pamoja na rais Milton Obote ambaye alikuwa na uhusiano mzuri sana na familia hiyo.

Wakati wakiwa katika vita kutaka kupindua serikali ya Obote, Muntu alipigwa risasi lakini akanusurika kifo na kutibiwa katika hospitali moja jijini Kampala.

Aliteuliwa kuwa kiongozi wa ujasusi katika jeshi la NRA, Museveni alipoingia madarakani mwaka 1986, ambapo alisaidiana na Paul Kagame ambaye baadaye alirejea Rwanda na kuwa rais.

Mafunzo ya kijeshi

Mugisha Muntu alipokea mafunzo ya kutosha ya kijeshi nchini Russia kabla ya kuwa kamanda wa jeshi kaskazini mwa Uganda.

Alipandishwa cheo na kuwa meja Generali katika jeshi la UPDF kabla ya kuteuliwa kuwa kamanda wa jeshi hilo.

Wachambuzi wanamtaja Mugisha Muntu kuwa msingi wa jeshi la sasa la Uganda na kamanda mwaminifu sana kwa rais Yoweri Museveni wakati alipokuwa anaongoza jeshi hilo.

Uaminifu huo ulifanya rais Yoweri Museveni akamuunga mkono kila kulitoa tofauti katika jeshi la Uganda hasa maafisa wa ngazi ya juu waliomshutumu kwa kujaribu kuwabagua.

Miongoni mwa maafisa hao ni marehemu meja Generali James Kazini.

Wakati wa utawala wake katika jeshi, Muntu alishutumiwa kwa kuwatenga maafisa ambao hawakuwa na elimu ya kutosha na kuwapendelea waliokuwa na elimu ya juu.

Muntu katika siasa

Alikuwa mwanachama wa bunge la kuandika katiba ya Uganda kati ya mwaka 1994 na 1995.

Aliondolewa kutoka uongozi wa jeshi la Uganda baada ya kutofautiana na mbinu za uongozi za rais Yoweri Museveni.

Aliteuliwa kuwa waziri lakini akakataa nafasi hiyo.

Mnamo Novemba 2001 alichaguliwa na bunge la Uganda kuwa miongoni mwa waakilishi 9 wa Uganda katika bunge la Afrika mashariki EALA.

Mugisha Muntu alioa Julia Kakonge Muntu mwaka 1992. Wana Watoto wawili. Mvulana na msichana.

Mugisha Muntu akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi.
Mugisha Muntu akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi.

Wachambuzi wa siasa wanamtaja Muntu kama kiongozi mwenye sifa nzuri, asiyependa fujo wala ufisadi.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG