Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 02:57

Wasifu wa mgombea nafasi ya urais Robert Kyagulanyi Sentamu


Robert Kyagulanyi akimsaidia mlinzi wake aliyejeruhiwa wakati wa ghasia kati ya wafuasi wake na vikosi vya usalama katika Wilaya ya Kayunga karibu na Kampala, Uganda, Dec. 1, 2020.
Robert Kyagulanyi akimsaidia mlinzi wake aliyejeruhiwa wakati wa ghasia kati ya wafuasi wake na vikosi vya usalama katika Wilaya ya Kayunga karibu na Kampala, Uganda, Dec. 1, 2020.

Robert Kyagulanyi Sentamu, maarufu kama Bobi Wine, ni mwanamuziki na mfanyabiashara aliyeingia kwenye siasa na wachambuzi wengi nchini Uganda wanasema anafanya bidii kujitegemea katika uchaguzi wa mwakana. 

Wanasema anafanya kila awezalo kupata fedha za kampeni bila ya msaada wowote wa wanasiasa wala wafanyabiashara maarufu.

Nyota yake ya siasa ilianza kung’aa mwaka 2017 kupitia uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Kyadondo wilayani Wakiso, karibu na Kampala.

Alipata ushindi mkubwa kwenye uchaguzi huo baada ya kugombania kama mgombea huru kufuatia chama cha FDC kukataa kumunga mkono na umaarufu wake katika siasa ukaanzia hapo.

Alichaguliwa kuwa mbunge wa Kyadondo mashariki, July 11 2017, na kuanzisha chama chake cha National unity platform NUP, ambapo wafuasi wake wanamtambua kama kiongozi wa watu wanaotaka mabadiliko nchini Uganda, maarufu kama People power, na wenye hisia kwamba wametengwa katika uongozi wa nchi hiyo, wengi wao wakiwa vijana.

Robert Kyagulanyi akiwa na mgombea urais kwa awamu nne Kizza Besigye katika mkutano wa waandisi wa habari Kampala
Robert Kyagulanyi akiwa na mgombea urais kwa awamu nne Kizza Besigye katika mkutano wa waandisi wa habari Kampala

Robert Kyagulanyi Sentamu, alizaliwa Februari tarehe 12 1982 katika hospitali ya Nkozi ambapo mamake ambaye ni marehemu alikuwa akifanya kazi.

Aliishi katika mtaa wa mabanda wa Kamokya jijini Kampala.

Alisoma katika shule tofauti ikiwemo shule ya upili ya Kitante Hill na shule ya upili ya Kololo, kabla ya kusomea muziki na uigizaji kiwango cha Diploma katika chuo kikuu cha Makerere na kumaliza mwaka 2003.

Alijiunga katika chuo kikuu cha Afrika Mashariki jijini Kampala mwaka 2016 na kusoma sheria.

Maisha yake ya Muziki

Kyagulanyi alijipatia jina la Bobi Wine, alipoanza muziki mapema mwaka 2000. Nyimbo zake za kwanza zilikuwa Akagoma , Funtula na Sunda, ambazo zilimpa umaarufu sana kote Afrika mashariki.

Wafuasi wa Bobi Wine wakionyesha mshikamano nje ya makazi yake Kampala mara baada ya kuwasili kutoka Marekani, Sept. 20, 2018.
Wafuasi wa Bobi Wine wakionyesha mshikamano nje ya makazi yake Kampala mara baada ya kuwasili kutoka Marekani, Sept. 20, 2018.

Muziki wake unaangazia sana maswala katika jamii na kutaka watu kuwa na subira, kuishi kwa amani wakiwa na matumaini ya kupata mafanikio maishani kwa kufanya kazi kwa bidii.

Lakini hivi karibuni amekuwa akiimba nyimbo za kutaka mabadiliko ya uongozi nchini, kutetea haki za kibinadamu na kutaka usawa katika jamii.

Alijiita kama rais wa vijana wanaishi maeneo ya mabanda vijijini. wafuasi wake wanamuita ‘Getho president.’

Ameandika na kuimba zaidi ya nyimbo 70 katika miaka 15 ya Muziki.

Muziki wake kwa jina Kiwani, ulitumika katika filamu ya malkia wa Katwe mwaka 2016. Bobi Wine pia aliigiza katika filamu mbalimbali nchini Uganda.

Bobi Wine katika siasa

Alipoingia kwenye siasa April 2017 Bobi Wine alikua anafanya kampeni yake kwa kutembea mlango hadi mlango wa wapiga kura sehemu hiyo kwa kukosa pesa za kuandaa kampeni.

Alishinda kiti hicho kwa kura nyingi, mara mbili zaidi ya wapinzani wake wote kama zimejumulishwa Pamoja.

Rais Yoweri Museveni alimfanyia kampeni mgombea wa NRM huku Dr. Kiiza Besigye akimfanyia kampeni mgombea wa FDC lakini Bobi Wine alishinda uchaguzi huo na hapo ndipo umaarufu wake wa kisiasa uliongezeka zaidi nchini Uganda.

Umaarufu wa Bobi wine katika siasa uliendelea kuongezeka, alipoongoza kampeni zingine katika uchaguzi mdogo katika sehemu mbali mbali za Uganda na wagombea aliokuwa akiwafanyia kampeni kushinda wagombea wa vyama vya NRM na FDC.

Agosti 14 2018, maafisa wa usalama walishambulia msafara wake na dereva wake akapigwa risasi, wakati alikuwa anamfanyia kampeni mgombea wa ubunge katika uchaguzi mdogo wa Arua.

Kyagulanyi alikuwa anafanyia kampeni mgombea huru Kassiano Wadri, dhidi ya mgombea wa chama cha NRM Nusura Tiperu. Wadri alishinda uchaguzi huo.

Kyagulanyi alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kutaka kupindua serikali yar ais Yoweri Museveni. Upande wa mashtaka ulidai kwamba alikuwa amepatikana na bunduki na risasi kadhaa. Ulidai vile vile kwamba wafuasi wake walikuwa wamepiga mawe msafara wa rais Yoweri Museveni.

Kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, mahajamani.
Kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, mahajamani.

Polisi na jeshi walidai kwamba alikuwa pia amepatikana na sare za jeshi. Baada ya siku chache baadaye, madai ya kupatikana na bunduki Pamoja na sare za kijeshi yaliondolewa bila maelezo zaidi ya bunduki zilizotajwa zilikuwa za nani na zilipotelea wapi.

Kesi dhidi yake ya kupindua serikali ilitupiliwa mbali na mahakama baada ya mwendesha mashtaka wa serikali kusema kwamba hakuwa na ushahidi kuendelea na kesi hiyo

Baadaye mwezi Agosti 2019, alifunguliwa mashtaka ya kumkasirisha rais Yoweri Museveni wakati wa machafuko yalitokea Arua mwaka mmoja kabla.

Bobi Wine kugombea urais

Mnamo tarehe 24 July 2019, Kyagulanyi alitangaza nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.

Tarehe 22 July 2020 alitangaza kuunda chama cha National unity platform NUP na kumteua mwandishi wa habari Joel Senyonyi kuwa msemaji wa chama hicho.

Hatua ya Bobi Wine kuwa na chama cha kisiasa ilifanyika kwa haraka na hata kuelekea mahakamani baada ya kudaiwa kwamba walimuuzia chama walifanya hivyo kinyume cha sheria lakini mahakama ilitupilia mbali kesi hiyo na kusema Bobi Wine alipata chama hicho kwa njia halali.

Iliripotiwa katika vyombo vya habari nchini Uganda kwamba rais Yoweri Museveni na viongozi wa chama kianchotawala cha NRM hawakufurahishwa na hatua ya Bobi Wine kuunda chama.

Tangu alipoingia katika siasa, Bobi Wine amekuwa na uhusiano mbaya na mwanamuziki mwenzake Bebe Cool ambaye amekuwa mfuasi mkubwa wa rais Yoweri Museveni. Bebe Cool amekuwa akimshambulia Bobi Wine kila mara kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vituo vya habari. Bobi Wine hata hivyo hajawahi kumjibu.

Bobi Wine (kulia) na binti yake Subi (L) wakati wa Chakula cha asubuli nyumbani kwake mjini Kampala, Uganda.
Bobi Wine (kulia) na binti yake Subi (L) wakati wa Chakula cha asubuli nyumbani kwake mjini Kampala, Uganda.

Familia ya Bobi Wine

Kyagulanyi ameoa Barbara Itungo. Wana Watoto wanne.

Jackson Wellington Ssentamu, aliaga dunia mwaka 2015 baada ya kuugua kisukari kwa mda mrefu.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA,Washington DC

XS
SM
MD
LG